Habari

Viongozi wataka Kiunjuri awe naibu wa Ruto 2022

October 8th, 2019 2 min read

Na STEVE NJUGUNA

VIONGOZI kadhaa kutoka Mlima Kenya wamependekeza Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri awe mgombea mwenza wa Naibu Rais William Ruto ifikapo mwaka wa 2022.

Wakizungumza katika uwanja wa michezo wa Nyahururu, Kaunti ya Laikipia, walimtaka waziri huyo aanze kuleta umoja miongoni mwa viongozi wa eneo hilo kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa miaka mitatu ijayo.

Viongozi hao wanaojumuisha Seneta wa Laikipia John Kinyua, Mwakilishi Mwanamke Cate Waruguru, Mbunge wa Laikipia Magharibi Patrick Makau na Spika wa Bunge la Kaunti Patrick Waigwa, walimtangaza waziri huyo kuwa mwanasiasa anayestahili kutwaa jukumu la kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa eneo hilo, na kuchukua mahali pa Rais Uhuru Kenyatta atakayestaafu urais kikatiba hapo 2022.

Kulingana nao, Bw Kiunjuri ana ujuzi mwingi wa kisiasa na hivyo basi anastahili zaidi kwa jukumu hilo muhimu.

“Kiunjuri amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 15. Amewahi pia kuwa waziri katika serikali tofauti kwa hivyo ana uwezo wa kuongoza eneo hili na kutupatia mwelekeo hata baada ya 2022,” akasema Bw Kinyua.

Viongozi hao walisema haifai kuwa na mwingine atakayependekezwa kuwa Naibu Rais isipokuwa Bw Kiunjuri.

“Tunamwomba Naibu Rais William Ruto ambaye tunaamini atapeperusha bendera ya Jubilee wakati wa Uchaguzi Mkuu 2022, ahifadhi nafasi ya mgombea mwenza kwa Waziri Kiunjuri,” akasema Bi Waruguru.

Wakati huo huo, walimwomba Bw Kiunjuri ajiepushe na siasa za mashinani na badala yake, aelekeze macho yake kwa siasa za kitaifa.

“Tunajua ana kila kinachohitajika kuwa Naibu Rais kwa sababu yeye ni kiongozi anayetambulika kitaifa,” akasema Bw Mariru.

Walikuwa wamehudhuria hafla ya kukabidhi wahudumu 200 wa bodaboda leseni kwa ufadhili wa Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF), ya eneobunge la Laikipia Magharibi.

Waziri huyo ambaye alikuwa mgeni mkuu katika hafla hiyo, alikana madai kwamba anapanga kuwania ugavana Laikipia ifikapo 2022. Aliomba viongozi wakomeshe siasa za mapema na badala yake waungane na Rais Kenyatta kutekeleza ahadi za maendeleo alizotolea Wakenya.

“Tunafaa kumuunga mkono Rais na naibu wake ili kuwe na maendeleo yanayostahili hasa kutekeleza ajenda nne kuu,” akasema.