Habari MsetoSiasa

Viongozi wataka Turkana igawanywe mara mbili

March 9th, 2020 1 min read

Na SAMMY LUTTA

VIONGOZI wa Kaunti ya Turkana wametangaza kuwa wanaunga Mpango wa Maridhiano (BBI) huku wakipendekeza kaunti hiyo igawanywe mara mbili.

Wakiongozwa na Gavana wa Kaunti hiyo Josphat Nanok, viongozi hao walisema kuwa BBI itasaidia eneo hilo ambalo lilikuwa limetengwa kwa muda mrefu kustawi kimaendeleo na muundomsingi ambao ndio uti wa mgongo wa uchumi.

Wengine waliokuwepo ni Waziri wa Madini na Mafuta John Munyes, Spika Ekitela Lokaale Seneta Malachy Ekal na wabunge Christopher Nakuleu (Turkana Kaskazini), James Lomenen (Turkana Kusini), Joyce Emanikor (Mwakilishi wa Kike), Jeremiah Lomorukai (Loima) na Mohammed Ali (Turkana Mashariki).

Kwenye taarifa ya pamoja, walisema eneo la Turkana limesalia nyuma kimaendeleo licha ya kuwa na asilimia 13 ya ardhi ya Kenya.

Bw Lodepe alisema kuwa Kaunti ya Turkana inafaa kugawanywa mara mbili na kila moja iwe na maeneobunge matatu.

“Tutahakikisha kuwa Kaunti ya Turkana inagawanywa mara mbili na tuongezewe maeneobunge na wadi,” akasema Bw Nanok.

Viongozi hao walisema kuwa mfumo wa ugatuzi umesaidia kupeleka maendeleo katika Kaunti ya Turkana hivyo wanataka kuhakikisha kuwa rasilimali zaidi zinapelekwa katika kaunti hiyo.

Kupitia taarifa yao ya pamoja iliyosomwa na Spika wa Bunge la Kaunti ya Turkana, viongozi hao walitaka serikali ya kitaifa inaanzisha miradi ya maendeleo katika maeneo yote nchini kwa usawa.

Viongozi hao pia walipinga matokeo ya sensa ya 2019 huku wakisema kuwa kaunti hiyo ina zaidi ya watu 1.3 milioni na wala si 926,976.

Walipinga pendekezo la kutaka kaunti kupewa mgao wa fedha kutoka kwa serikali ya kitaifa kwa kuzingatia idadi ya watu.

“Tunafaa kuendeleza kanuni za sasa ambapo fedha zinatolewa kwa kuzingatia ukubwa wa eneo,” akasema Bw Ekitela.

Alisema kuwa baadhi ya kaunti zilizo na idadi kubwa ya watu tayari zimestawi kimaendeleo hivyo haitakuwa sawa kutengewa kiasi kikubwa cha fedha.

Turkana ni mojawapo ya kaunti ambazo ni kubwa zaidi na zinahitaji kutengewa kiasi kikubwa cha pesa.