Habari Mseto

Viongozi wawahimiza wakazi wa Thika wakubali BBI, baadhi wakisema viti zaidi ni mzigo

December 4th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI wametoa maoni yao kuhusu ripoti ya BBI, Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, akisema asilimia kubwa ya ripoti hiyo iko sawa na kwa hivyo ni bora wananchi waikubali.

“Hiyo sehemu kubwa nzuri inastahili kuungwa mkono na kila mmoja hapa nchini,” alisema Bw Wainaina.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi katika kijiji cha Githima, Munyu Thika Mashariki alipohudhuria mazishi ya mama mkwe wa Mbunge wa Kiambu Bw Jude Njomo.

Hata hivyo kile anachopinga ni kuongezwa kwa viti vya wabunge 70 zaidi akisema huo ni mzigo kwa mwananchi wa kawaida.

“Kwa wakati huu nafasi za kuketi kwa viongozi bungeni ni chache, ambapo kunastahili kuweka mahali pakubwa pa kutosha viongozi zaidi watakaochaguliwa,” alisema Bw Wainaina.

Alisema iwapo itabidi wabunge zaidi waongezwe, “ni sisi viongozi tukatwe mishahara yetu ili kugharimia mzigo huo wa mshahara.”

“Mimi nitakuwa mstari wa mbele kukatwa nusu ya mshahara wangu ili kuonyesha umuhimu wa yale ninayosema,” alifafanua mbunge huyo.

Aliwarai watu wa Mlima Kenya wawe mstari wa mbele kuiunga mkono ripoti hiyo kwa sababu inawanufaisha zaidi.

Mbunge wa Gatundu Kusini ambaye pia aliandamana na mbunge mwenzake Wainaina, Bw Moses Kuria, alisema ripoti ya BBI ni ya kuongeza mwananchi mzigo.

“Ripoti hiyo haifai kuongeza viti zaidi kwa sababu tayari mwananchi amelemewa na mizigo mizito. Hata uchumi wa nchi hii imethibitishwa kuwa iko katika hali mbaya,” alisema Bw Kuria.

Alimtaka rais Uhuru Kenyatta kuacha msingi nzuri wa kiuchumi badala ya kumwacha ‘ Wanjiku’ katika hali ya shida.

Alisema wananchi wanapitia masaibu mengi kama homa ya covid-19, wazazi wanajiandaa Januari kupeleka watoto wao shuleni, huku akidai ni mzigo mzigo mkubwa.

Alisema kura ya maoni itagharimu fedha nyingi ambapo hatua hiyo inastahili kuambatana na uchaguzi wa 2022.

Askofu mkuu wa Calvary Church mjini Thika Bw David Ngari Gakuyo, alisema watu wa Mlima Kenya wanastahili kuwa wazi na kuiunga ripoti hiyo kwa sababu inawanufaisha pakubwa.

“Iwapo watu wa Mlima Kenya bado wanaendelea na mtindo wao wa kupinga ripoti hiyo basi wana ubinafsi ndani yao ama hawajielewi ni nini wanachotaka,” alisema Askofu Gakuyo.

“Tunastahili kuipitisha ripoti hiyo mara moja kwa sababu tunataka kuona suala la ufisadi likitatuliwa vilivyo. Wale wanaoipinga wana jambo fiche ambalo wanalielewa huku lengo lao likiwa kuwa katika mrengo wa kupinga ripoti hiyo,” alisema mchungaji huyo.

Alisema Rais Uhuru Kenyatta ana maono makubwa ndiyo maana anataka kuhakikisha Wakenya wote wanaishi kwa amani bila kusumbuliwa na yeyote.

Alitoa ushauri kwa mrengo wa Tangatanga kujitokeza wazi na kueleza Wakenya ni nini wanachotaka kwa sababu hawana msimamo maalum.

“Tunataka tuwe na viongozi walio na msimamo wa kuonekana wala sio kutumia mbinu za kupotosha Wakenya bila kuwa na mwelekeo mmoja,” akasema Askofu huyo.