Viongozi, wazee watofautiana kuhusu Raila

Viongozi, wazee watofautiana kuhusu Raila

Na OSCAR KAKAI

MGOGORO unatokota kati ya kundi la viongozi wa jamii ya Wapokot na Baraza la Wazee wa jamii ya Pokot ambao wamejitokeza kwa hasira kuhusu hatua ya hivi majuzi ya kuidhinisha azma ya urais ya Kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga, 2022.

Hii ni baada ya Gavana wa Pokot Magharibi, John Lonyangapuo, Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing , mbunge wa zamani wa Tiaty Asman Kamama ambao wameunda chama kipya cha Kenya Union Party (KUP) na Kiongozi wa Wengi katika Seneti Samuel Poghisio (Kanu) kutangaza kumuunga mkono Bw Odinga katika hafla ya Azimio la Umoja iliyofanyika kwenye Uwanja wa Maonyesho wa Kishaunet, Kapenguria, Jumatatu.

Viongozi wa KUP waliwasilisha walichotaja kama maafikiano ya watu kwa Bw Odinga na wakaahidi kufanya kazi naye.Hata hivyo, Baraza la Wazee wa Jamii ya Pokot, kundi linalofanya maamuzi makuu kuhusu uongozi wa jamii hiyo, lilisema uamuzi wa Gavana Lonyangapuo na Mbunge Pkosing wa kumwidhinisha Bw Odinga na kuunda chama kingine, ulikuwa njia ya kukwepa kesi zinazowakabili kuhusu madai ya ufisadi.

Wakizungumza na Taifa Leo mjini Kapenguria, wazee hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo John Muok walipuuzilia mbali hatua hiyo wakiitaja kama shughuli ya watu wawili na kusisitiza kwamba hawakuhusishwa.Bw Muok alionya kuhusu wanaotaka jamii ya Wapokot kuwa na utambulisho wake na kujitenga na jamii ya Wakalenjin akisema wanasiasa hawana mamlaka ya kuzungumzia suala hilo kwa niaba ya jamii.

“Nani aliwaambia wao ni wasemaji wa jamii. Hakuna chochote kuwa Wapokot si Wakalenjin. Wamepotoka,” alisema Mzee Muok.

You can share this post!

Mlipuko waangamiza watu wanane Somalia

Ruto, Raila wakoroga chama cha Kingi PAA

T L