Michezo

Vipaji vipya vya Gor vyaisaidia kuzima Kariobangi Sharks

February 26th, 2018 2 min read

Sajili mpya wa Gor Mahia Samuel Onyango (kushoto) katika mechi dhidi ya Nakumatt Fc. Picha/ Maktaba

Na GEOFFREY ANENE

SAJILI wapya Samuel Onyango na Ephrem Guikan wamefungia Gor Mahia bao moja kila mmoja na kuisaidia kudumisha kubwaga Kariobangi Sharks 2-1 kwenye Ligi Kuu, Jumapili.

Onyango, ambaye alisajiliwa kutoka Ulinzi Stars, aliona lango dakika ya 10 kabla ya kipa wa Gor, Boniface Onyango kufungwa bao rahisi kupitia frikiki ya Bolton Omwenga alipokosa kumakinika na kufungwa katikati ya mguu yake.

Raia wa Ivory Coast alihakikishia mabingwa watetezi Gor ushindi alipopachika bao la pili dakika ya 70. Ushindi huu wa Gor ni wa tatu mfululizo msimu huu na pia dhidi ya Sharks.

Walipepeta Sharks 3-1 Machi 12 na kuidunga tena 3-1 Oktoba 17 mwaka jana. Msimu huu, Gor ilivuna pointi tatu kutoka kwa Nakumatt na pia Zoo Kericho kwa kuzipepeta 4-0 na 4-2, mtawalia. Kichapo hiki nacho ni cha kwanza kwa Sharks ambayo ilipiga Nzoia Sugar 1-0 kabla ya kukabwa 2-2 na Vihiga United na 1-1 dhidi ya Chemelil Sugar.

Leopards iliandikisha ushindi wake wa kwanza msimu huu na wa pili mfululizo dhidi ya Ulinzi Stars kwa kuizaba mabao 2-1 uwanjani Thika.

Mathare iilizoa ushindi wa tatu msimu huu kwa kuilima Sofapaka 3-1 uwanjani Machakos nayo Zoo ikatoka nyuma 1-0 na kufuta vichapo vitatu ilivyopokea kutoka kwa Ulinzi, Gor Mahia na SoNy Sugar kwa kulemea Thika United 2-1 ugani Kericho Green.

Bao la kwanza la Ingwe liliwasili baada ya Jaffery Awiti kupokea krosi safi kutoka kwa Brian Marita na kupitisha mpira juu ya kipa wa Ulinzi, Timothy Odhiambo dakika ya 69.

Ulinzi ilisawazisha 1-1 kupitia ikabu ya Oliver Ruto dakika kumi baadaye kabla ya Marvin Nabwire kufungia mabingwa mara 13 Leopards bao la ushindi sekunde ya mwisho baada ya kutokea kizaazaa langoni mwa mabingwa mara nne, Ulinzi Stars.

Mabingwa wa mwaka 2008, Mathare, walizima mabingwa wa 2009, Sofapaka kupitia mabao ya Francis Omondi, Chrispin Oduor na Edward Seda.

Baada ya mashambulizi makali kutoka kwa klabu hizi mapema, Mathare ya kocha Francis Kimanzi ilifanikiwa kuona lango ya kwanza.

 

Penalti

Refa Peter Waweru aliipa Mathare penalti baada ya Rodgers Aloro wa Sofapaka kuangusha Seda ndani ya kisanduku dakika ya 17. Omondi alifuma penalti safi kwa kumwaga kipa Mganda Mathias Kigonya.

Oduor aliimarisha uongozi wa Mathare dakika ya 27 alipochota mpira juu ya Kigonya.

Sofapaka iliendela kuvamia ngome ya Mathare na kufaulu kupunguza mwanya huo hadi 2-1 dakika ya 42 kupitia penalti iliyopigwa na Kigonya. Johnstone Omurwa alinawa mpira ndani ya kisanduku chao na kumpa Kigonya nafasi ya kumfunga Robert Mboya.

Ufufuo wa Sofapaka ulizimwa Seda alijazia Mathare goli la tatu wavuni dakika ya 63.

Licha ya kupiga dakika 28 za mwisho watu 10 baada ya Nicholas Kipkurui kulishwa kadi nyekundu kwa kucheza visivyo, Zoo ilinyamazisha Thika 2-1. Clement Masakidi alifungia Thika katika dakika ya 31 kabla ya Zoo kujibu kupitia Michael Madoya na Geoffrey Gichana.

Matokeo:

Februari 25

Mathare United 3-1 Sofapaka

AFC Leopards 2-1 Ulinzi Stars

Zoo Kericho 2-1 Thika United

Kariobangi Sharks 1-2 Gor Mahia

Februari 24

Tusker 2-1 Nzoia Sugar

Bandari 1-0 Wazito

Kakamega Homeboyz 2-1 Vihiga United

Posta Rangers 1-0 Chemelil Sugar

Nakumatt 0-0 SoNy Sugar