Michezo

Vipaji vyachochea KPL kuanzisha ligi kuu ya wafungwa

September 11th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

Baada ya kupata kuna talanta ya hali ya juu inayoozea katika majela ya Kenya, kampuni ya KPL, ambayo inaendesha Ligi Kuu ya soka nchini, imeamua kuanzisha Ligi Kuu ya wafungwa.

Taarifa kutoka KPL zinasema kwamba kampuni hii imeshirikiana na shirika la Zeb Strong Foundation kuanzisha ligi ya wachezaji saba kila upande almaarufu kama Inmates Premier League.

Ligi yenyewe itajumuisha klabu 25. Jela ya Kamati Maximum itakuwa na ligi ya klabu 13 nayo ligi ya Naivasha Maximum ikikutanisha klabu 12.

Uzinduzi wa ligi hii ulifanywa Septemba 5, 2018 katika jela ya Kamiti ambapo mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya AFC Leopards walilazimishwa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Kamiti All Stars katika mechi ya kusisimua ya kirafiki ya wachezaji saba kila upande.

Katika uwanja wa moramu na kokoto, Kamiti All Stars iliongoza 3-1 wakati wa mapumziko kabla ya Ingwe kujikakamua na kusawazisha 3-3 katika kipindi cha pili.

Lengo kubwa la kuanzishwa kwa ligi hii ni kuwapa wafungwa tumaini na shughuli isiyo ya kihalifu pamoja na kuwarekebisha kabla ya kukamilisha vifungo vyao. Wafungwa wengi katika majela haya mawili wanatumikia vifungo vya zaidi ya miaka 10.

Orodha ya timu za Inmates Premier League hii hapa chini:

Kamiti Maximum – Academica FC, Academy FC, Alaska FC, Alaska Jnr FC, Black Star FC, Blue Sky FC, Gunners FC, Hamas FC, Kadhiani FC, M.O.G FC, Mathare FC, Morocco FC na Taqwa FC.

Naivasha Maximum – Arsenal FC, AS Monaco FC, Atletico Madrid FC, Barcelona FC, Bayern Munich FC, Celtic FC, Chelsea FC, Dragon FC, Everton FC, Juventus FC, Olympic FC na Real Madrid FC.