Makala

‘Vipepeo weupe waashiria dalili za mwaka wa baraka’

February 7th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

MCHIPUKO wa maelfu ya vipepeo weupe katika sehemu tofauti nchini umeibua msisimko na hisia tofauti miongoni mwa Wakenya, kwani hali hiyo inatajwa kuwa tukio nadra sana kutokea.

Vipepeo hao wamekuwa wakishuhudiwa katika kaunti tofauti kama Nairobi, Nyeri, Kirinyaga, Nyandarua kati ya nyingine.

Wamekuwa wakipaa huku wakiandamana na upepo.

Katika Kaunti ya Nyandarua, vipepeo hao wamekuwa wakishuhudiwa kwenye vichaka na maeneo ya kuwalisha mifugo.

Vipepeo weupe wakionekana kwa umbali katika kijiji cha Kieni, Kaunti ya Nyandarua. PICHA | WANDERI KAMAU

Katika kijiji cha Kieni, kilicho katika Kaunti ndogo ya Ndaragwa, Kaunti ya Nyandarua, wanakijiji walieleza hisia tofauti kuhusu tukio  hilo la kipekee.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bi Mary Nyawira alitaja tukio hilo kama “ishara na dalili ya baraka”.

“Kwa kawaida, mwezi wa Januari huwa umekauka. Huwa mwezi wa jua kali, ambapo wanakijiji wengi huwa mashambani mwao, wakiyatayarisha kwa msimu wa mvua ya masika ambayo kwa kawaida huwa inaanza kutoka Machi hadi Mei. Huwa nadra sana kuwaona vipepeo kama hao. Kulingana na simulizi niliyopewa na nyanya yangu, tukio hili linaashiria mwaka wa baraka,” akasema Bi Nyaruai, aliye miongoni mwa wanakijiji walioeleza kushangazwa na tukio hilo.

Mwanakijiji mwingine, Bw Duncan Ndung’u, alikubaliana na kauli hiyo, akisema kuwa kwa kawaida, vipepeo kama hao hushuhudiwa msimu wa mvua na ni nadra sana kwao kutokea wakati wa kiangazi.

“Vipepeo huwa wanatokea tu wakati wa mvua ya masika. Ni sadfa kubwa kuwa kando na vipepeo hao, kuna mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha. Bila shaka, hii ni ishara na utabiri wa mapema kwamba huu utakuwa mwaka wa baraka,” akasema Bw Ndung’u.

Wazee kadhaa waliozungumza na Taifa Leo walitaja tukio hilo kuwa “sauti kutoka kwa Mungu”, kwamba wanakijiji hao na Wakenya  kwa jumla wanafaa kujitayarisha kwa “mwaka wa baraka”  baada ya 2023 kuwa mwaka mgumu kwa watu wengi.

“Hii ni sauti ya Mungu. Ni sauti ya kuwafariji watu wetu kwamba huu ni mwaka watakaopata mavuno mengi baada ya kupitia hali ngumu mwaka 2023,” akasema Mzee Thiong’o wa Gichuni.