Michezo

Vipers ya Wafula yaing'ata Onduparaka

January 9th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Innocent Wafula aliwasili katika Vipers SC na kismati baada ya ?mabingwa hawa watetezi kuandikisha ushindi wao wa kwanza katika mechi tatu kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uganda kwa kucharaza Onduparaka FC 2-0 uwanjani St Mary’s Kitende, Jumanne.

Vipers ilikuwa imekabwa 0-0 dhidi ya Tooro United na pia kuumiza nyasi bure katika sare tasa dhidi ya Bright Stars katika mechi mbili zilizotangulia.

Wafula alisajiliwa Januari 6, 2019 na mabingwa hawa wa Uganda mwaka 2009/10, 2014/15 na 2017/18 na kuanzishwa dhidi ya Onduparaka.

Winga huyu, ambaye pia ni beki wa pembeni kushoto, aliachiliwa na Gor Mahia baada ya kupoteza namba yake kwa wachezaji Philemon Otieno, Wellington Ochieng na sajili mpya Pascal Ogweno.

Jumanne, alipoteza nafasi ya kuipa Vipers uongozi dakika ya 33 baada ya kumegewa krosi murwa na Yayo Lutimba, huku dakika 45 za kwanza zikitamatika bila bao.

Hata hivyo, dakika tatu baada ya kipindi cha pili kuanza, Geoffrey Wasswa aliweka Vipers bao 1-0 juu kabla ya mvamizi wa zamani wa Gor, Dan Sserunkuma kuongeza bao la pili dakika ya 52. Livingstone Mulondo alihitimisha dakika ya 72 baada ya Lutimba kuchota kona safi.

Wafula amesaini kandarasi ya miaka mitatu na klabu hiyo ya Uganda, ambayo iliajiri kocha Mkenya Michael ‘Nam’ Ouma mnamo Desemba 30, 2018 baada ya kutimua raia wa Mexico Javier Martinez Espinoza.

Ushindi huu ni wa kwanza wa Ouma, ambaye alishuhudia vijana wake wakikabwa 0-0 dhidi ya Bright Stars mnamo Januari 5 ugenini. Unaimarisha pointi za nambari mbili Vipers hadi 29 kutokana na mechi 13 kwenye ligi hii ya klabu 16. Mabingwa mara 12 Kampala City wanashikilia uongozi. Onduparaka imeteremka chini nafasi moja hadi nambari nne baada ya kichapo kutoka kwa Vipers.