Makala

TUONGEE KIUME: Vipusa hawavutiwi na hela pekee, wanataka kutunzwa kama malkia

Na BENSON MATHEKA August 12th, 2024 2 min read

HAWA vipusa mnaoona wanajua wanachotaka kwa mwanamume na ikiwa unadhani ni pesa pekee zinazowachangamsha unakosea. 

Kipusa anayethamini uhusiano wa kimapenzi anazamia vitu kadhaa kabla ya kufikiria kumeza chambo kwa sababu ya pesa.

Kaka, ukiwa mbumbumbu, utakula kwa macho.

Vipusa wa kisasa wanapima akili ya mwanamume kabla ya kuwazia kuhusiana naye.

Hakuna mwanamke anayetamani kuhusishwa au kuhusika na mwanamume mwenye akili maziwa lala.

Ikiwa hakuna kitu kichwani mwako isipokuwa soka ya ulaya na ngono, usichoke kusumbua vidosho.

Mwanamume mwenye akili huwa mtanashati. Sio lazima avalie suti na jezi kutoka ulaya.

Ni mtu anayetunza nywele na mavazi yaliyopigwa pasi nadhifu pamoja na mchanganyiko bora wa rangi. Kaka, kujipanga ni muhimu.

Usiwahi kuweka mbele mwanadada kuliko kazi au biashara yako. Atakuambaa.

Akina dada wanadharau mwanamume asiyechukulia kazi au biashara yao kwa uzito.

Wanasema mapenzi hayajazi tumbo. Kabla ya kuwazia kurushia demu ndoano, lazima ujiamini.

Uwe na ujasiri hata kama hatameza chambo. Na usiwe mtu wa kurushia maneno ovyo ovyo.

Fikiria kabla ya kuachilia neno. Achilia maneno kwa hekima, ujuzi na ufahamu. Usizungumze uonekane unajua kuzungumza.

Utani wa kijinga na mijadala isiyo na maana ni ya watu wavivu, wasio na maono.

Kama huna lolote la busara la kusema funga mdomo wako. Kila mwanamke hupenda mwanaume anayeweza kumtegemea.

Usitamani kipusa mtaalamu ikiwa wewe ni kabwela wa mtaani.

Utaumia bure kaka. Hakuna makosa kurudi shuleni kujinoa uweze kuwania vipusa waliofanikiwa. Bidii kaka, bidii.

Hakuna kipusa mwenye akili timamu anayeweza kupuuza mwanamume mwenye akili, mtanashati, anayejiamini na anayejitolea kwa asilimia 100 katika kazi, biashara, huduma na mwenye maono.

Haya yote huleta pesa ambazo wengi husema vipusa wanapenda.

Naam, huo ndio ukweli, pesa ni kichocheo namba moja cha mapenzi.

Ukikosa pesa wanawake watakuwa baridi kwako. Ukiwa nazo na uwe mkono birika, usiwazie kurushia vipusa mistari.

Vidosho wa kisasa wanapenda wanaume wakarimu.

Ikiwa wewe ni kubana, hakuna mwanamke mwenye akili timamu atakayekuvumilia.

Kabla ya kumkaribia mwanamke yeyote, piga mswaki meno yako. Wekeza kwenye manukato mazuri tafadhali!

Ukifanya hivi, toka, ingia sokoni na vipusa watakupigania.

Vipusa wanapagawishwa na machali wanaotabasamu, wanaovutia kila siku, wakati wowote.

Kaka, jifunze jinsi ya kumfanya mwanamke ajisikie vizuri, jifunze kufanya utani safi na mzuri.

Tabasamu na kucheka kunakufanya upendeze sana. Onyesha adabu na heshima kwa wanawake.

Jifunze kuvutia demu kiti akae, ukifungua mlango mwache aingie kwanza.

Mchukulie kama malkia na utamyeyusha moyo haraka. Usiwe mkorofi na mkali bila sababu.

Hakuna demu anayetaka kuolewa na mwanaume wa aina hiyo.