Michezo

Vipusa sasa kumkamatia chini bondia Mayweather

July 28th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MIEZI michache baada Floyd Mayweather kupata hifadhi mpya ya penzi lake moyoni mwa mwanamitindo chipukizi Yasmi Mendeguia, mwanandondi huyo maarufu mwenye umri wa miaka 42 amejipata pabaya.

Hii ni baada ya vichuna wawili kujitokeza na kudai kwamba wana ujauzito wa bondia huyo aliye na historia ya kutoka kimapenzi na vipusa wa kila sampuli.

Melissa Brim aliyewahi kusalitika kimapenzi kwa Mayweather amesema anatarajia mtoto wa kiume kufikia mwisho wa mwaka huu. Kidosho huyu aliwasha upya mwenge wa penzi lake kwa Mayweather mnamo Februari mwaka huu.

Mbali na Melissa, kichuna mwingine ambaye kwa sasa kabebeshwa tumbo na Mayweather ni Dolarie Medina ambaye amekuwa akitamani sana kurudiana kimapenzi na mwanamasumbwi huyu ili kuzima azma ya Yasmi kwa dume hili linalomezewa pia ni Josie Harris aliyewahi kulizalia watoto wawili wa kiume.

Zaidi ya Josie, Yasmi ambaye kwa sasa anamfungulia Mayweather buyu la asali yake, warembo wengine ambao wamefunguka na kukiri kunyemelewa upya na staa huyu ni Jessica Burciaga, Shantel Jackson na Abi Clarke.

Mayweather amewahi pia kutoka kimapenzi na vichuna Liza Hernandez, Raemarni Ball na Jennifer Duran aliyemzalia mtoto wa tano mwaka jana.

Koraun na Zion ni watoto wawili wa kiume ambao Mayweather aliwapata baada ya kuhusiana na Josie kwa zaidi ya miaka sita. Uhusiano wake na ? Melissa ulimpa wasichana wawili – Iyanna na Jirah.

Kulingana na gazeti la The Sun, kiini cha Melissa kutaka sana kurudiana na bondia huyu si tu weledi wake katika masuala ya chumbani, bali pia wingi wa hela zinazojivuniwa na ‘Money Man’.

Melissa anafahamika sana kwa mazoea ya kujilegeza kirahisi kwa wanamichezo maarufu na hata wanaspoti chipukizi wenye vipochi vya hela nyingi. Miezi minne iliyopita, Yasmi, 22, alipakia mtandaoni picha alizopigwa kwa pamoja na Mayweather na hivyo kuanika ukubwa wa kiwango cha kukomaa kwa penzi lao.

Kulingana naye, sadfa ilimkutanisha na dume hilo katika mojawapo ya maduka makuu jijini Los Angeles, Amerika mwishoni mwa Machi 2019. Baada ya kupiga picha za pamoja, Mayweather aliyenakili nambari ya simu ya kidosho huyo alianza kumtumia picha, video na jumbe za kumtaka kimapenzi.

“Nilikuwa na baadhi ya wenzangu dukani. Nilimuona Mayweather na nikamwendea kwa nia moja ya kupiga naye picha,” akatanguliza.

“Baadaye tulianza kuwasiliana mara kwa mara na tukapanga kukutana nchini Mexico alikopata fursa ya kuonja tunda, akaridhishwa na ustadi wangu wa Kupiga miereka chumbani,” akaongeza Yasmi.

Zaidi ya kuwa mwanamitindo, Yasmi aliyewania taji la Big Brother nchini Uhispania mnamo 2016, pia ni mwigizaji na msakataji wa densi.