Vipusa wa Barcelona wapokeza Arsenal kichapo cha kwanza tangu Februari 2021

Vipusa wa Barcelona wapokeza Arsenal kichapo cha kwanza tangu Februari 2021

Na MASHIRIKA

ARSENAL walipoteza mechi kwa mara ya kwanza tangu Februari 2021 baada ya mchezaji wao wa zamani, Asisat Oshoala kuongoza Barcelona kuwatandika 4-1 katika mchuano kufungua kampeni za Kundi C kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Barcelona waliwekwa kifua mbele na Mariona Caldentey aliyekamilisha krosi ya Oshoala katika dakika ya 31 kabla ya Alexia Putellas kufunga bao la pili kunako dakika ya 42 baada ya kushirikiana tena na Oshoala ambaye ni raia wa Nigeria.

Oshoala mwenyewe alipachika wavuni goli la tatu mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya kuandaliwa pasi nzuri na Mariona.

Ingawa Frida Maanum alipania kurejesha Arsenal mchezoni katika dakika ya 74, chombo chao kilizamishwa kabisa na Lieke Martens aliyefungia Barcelona bao la nne kunako dakika ya 84.

Putellas angalifanya mambo kuwa 5-1 mwishoni mwa kipindi cha pili lakini penalti yake ikapanguliwa na kipa Manuela Zinsberger.

Oshoala, 26, alichezea Arsenal kuanzia Machi 2016 hadi Februari 2017 na kuwasaidia kunyanyua Kombe la FA. Hivyo, hakusherehekea bao alilowafunga waajiri wake hao wa zamani mnamo Jumanne usiku uwanjani Johan Cruyff.

Iliwachukua Arsenal dakika 55 kabla ya kuelekeza kombora langoni mwa Barcelona japo fataki hiyo kutoka kwa Vivianne Miedema ikadhibitiwa vilivyo na kipa Sandra Panos. Mbali na Miedema, mchezaji mwingine wa Barcelona aliyemtatiza Sandra ni Nikita Parris.

Chini ya kocha Jonas Eidevall, Arsenal walishuka dimbani kwa ajili ya mchuano huo wakipigiwa upatu wa kusajili matokeo bora ikizingatiwa ubora wa fomu yao katika mechi za awali ambapo walishinda mechi nane kutokana na michuano minane ya mashindano yote.

Arsenal waliokuwa wamefunga wastani wa mabao matatu katika kila mchuano kabla ya kuvaana na Barcelona, walipigwa kwa mara ya mwisho mnamo Februari 2021 na hawakuwa wamepigwa kutokana na mechi 20.

Vipusa wa Arsenal watakuwa wenyeji wa Hoffenheim ya Ujerumani katika mchuano wao ujao kundini mnamo Oktoba 14, 2021 huku Barcelona wakitua Denmark kumenyana na Koge. Hoffenheim walitandika Koge 5-0 katika mchuano mwingine wa Kundi C mnamo Oktoba 5, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wakazi walia daraja bovu na ahadi hewa

Familia ya Glazer kuuza hisa 9.5 milioni za Man-United kwa...