Vipusa wa Joylove wanataka kurejea ligi ya daraja la kwanza

Vipusa wa Joylove wanataka kurejea ligi ya daraja la kwanza

Na JOHN KIMWERE

TIMU za michezo huanzishwa kwa malengo tofauti ikiwamo kukuza vipaji vya chipukizi ili kuibuka wachezaji wa kimataifa miaka ijayo.

Katika soka waasisi wengi hupania kutumia ujuzi wao kujenga vikosi imara kushiriki Ligi Kuu pia kuona baadhi ya wachezaji wao wakiiva na kutinga kiwango cha kusakatia timu za taifa.Kinyume na miaka iliyopita michezo imeibuka kitego uchumi kwa wengi wanaume na wanawake.

Joylove Academy ni kati ya vikosi vya soka ya wanawake vinavyokuza wachezaji chipukizi nchini. ”Nilianzisha timu hii nikilenga kuleta pamoja wachezaji chipukizi hasa wasichana kunoa vipaji vyao angalau wafanikiwe kushiriki soka la kimataifa siku zijazo,” anasema Joyce Achieng aliye mwanzilishi na kocha mkuu wa vikosi vya wavulana na wasichana vilivyo chini ya kituo hicho.

Anasema soka husaidia wengi wachezaji chipukizi kupata ufadhili wa elimu ya Shule za Upili bila kuweka katika kaburi la sahau kuwa ni ajira. Kando na hayo soka imeajiri wengi kote duniani. Joylove FC inayoshiriki kampeni za soka la Central Regional League (CRL) inalenga kupigana mithili ya mchwa kuhakisha inabeba tiketi ya kurejea kushiriki mechi za Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza muhula ujao.

Picha/JOHN KIMWERE
LOVE:Timu ya Joylove FC

”Sekta ya michezo nchini inahitaji ufadhili ili timu kuendeleza jukumu la kukuza chipukizi wanaokuja. Sina budi kutaja kuwa ufadhili umeibuka donda sugu kwa timu za michezo tofauti. Anaatoa wito kwa wahisani wajitokeza na kufadhili vikosi vya michezo mashinani ili kutimiza azma ya wachezaji wengi ambao hutamani kushiriki soka la kulipwa ughaibuni.

Ninashiriki kipute hicho baada ya kuteremshwa daraja tulipomaliza wa mwisho katika Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza msimu uliyopita. Tumefungua kampeni zetu kwa ushindi tunakolenga kuendeleza mtindo huo na kumaliza mechi zote bila kushindwa ili kujikatia tiketi ya kusonga mbele.

” Kwenye mechi ya ufunguzi, Joylove chini ya nahodha, Sharon Khasandi ilivuna ufanisi wa goli moja mtungi mbele ya Gikambura Starlets ugani Gikambura Stadium, Kikuyu.Anashikilia kuwa anatamani sana kuona timu yake ikifaulu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu ya Soka la Wanawake(KWPL) jambo analolenga kutimiza ndani ya miaka mitatu ijayo.

Mwaka jana alianzisha timu za wavulana viwango vya (U-10), (U-12) na (U-14) ambavyo hufanyia mazoezi katika uga wa Shule ya Msingi ya Gatina. Nao wasichana hutumia uwanja wa Chuo cha Walimu cha Thogoto, Kikuyu.

Timu hii ilibuniwa mwaka 2015 imefaulu kulea vigoli wachache akiwamo Vivian Awuor (Kibera Soccer Ladies) na Nancy Wafula (Soccer Sisters) za Ligi Kuu (KWPL) na Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza mtawalia.

Vigoli hao wanajivunia kuibuka mabingwa wa Ligi ya Kaunti Ndogo ya Mkoa wa Kati bila kushindwa pia kutawazwa bingwa wa ngarambe ya CRL mwaka 2018.Katika kipute cha CRL Joylove imepangwa Kundi A linalojumuisha: Kikuyu Chicks,Gikambura Starlets, Joylove FC, Galaxy FC, Zoe Unify FC, Cardinal FC, Limuru Queens FC, Maraba Queens FC na Thirime Queens FC.

Timu hii imeundwa na wachezaji hawa:Sharon Khasandi (kipa na nahodha), Beryn Migalusha na Vella Chairo ( wasaidizi wa nahodha), Mercy Ayuma, Lilian Muthoni, Eunice Bosibori, Vella Chairo, Ruth Nekesa, Cynthia Zindori, Halima Melisa, Farida Wambui, Consolata Mbechi, Faith Achieng na Snorine Anzika. Pia wapo Ruth Wekesa, Cynthia Atieno, Resah Naliaka, Bethel Aluoch, Patience Khasiala, Brenda Atieno, Phanice Ayuma, Juliana Mwende na Mercy Nekesa

  • Tags

You can share this post!

SONIA: Chipukizi anayelenga nyayo za Priyank Chopra

Everton wasajili fowadi Andros Townsend na kipa Asmir...