Vipusa wa Uingereza wapiga Ujerumani na kutwaa taji la Euro 2022

Vipusa wa Uingereza wapiga Ujerumani na kutwaa taji la Euro 2022

Na MASHIRIKA

WAREMBO wa Uingereza waliandikisha historia kwa kushinda taji la kwanza la mapambano ya haiba kubwa miongoni mwa wanawake baada ya kukomoa Ujerumani 2-1 katika fainali ya Euro 2022 mnamo Jumapili ugani Wembley.

Chloe Kelly aliyerejea ugani kusakata soka mnamo Aprili baada ya jeraha la goti kumweka nje kwa miezi 11, alifungia Uingereza bao la ushindi katika muda wa ziada.

Alifuta juhudi za Lina Magull aliyesawazishia Ujerumani baada ya Ella Toone kufungua ukurasa wa mabao. Gozi hilo lilivutia mashabiki 87,192 uwanjani – idadi ya juu zaidi ya watu kuwahi kuhudhuria fainali ya Euro kwa upande wa wanawake au wanaume.

Uingereza walishinda Ujerumani miaka 56 baada ya kikosi chao cha wanaume kupepeta West Germany 4-2 katika fainali ya Kombe la Dunia mnamo 1966. Hadi kufikia Jumapili, taji hilo ndilo la pekee lililokuwa likijivuniwa na Uingereza kwenye mashindano ya haiba miongoni mwa wanawake na wanaume.

Sarina Wiegman anayenoa vipusa wa Uingereza, pia aliingia kwenye mabuku ya historia kwa kuwa kocha wa kwanza kuwahi kunyanyua taji la Euro mara mbili mfululizo akidhibiti mikoba ya vikosi tofauti. Mkufunzi huyo aliongoza Uholanzi kutandika Denmark 4-2 katika fainali ya Euro 2017.

Kiungo wa Ujerumani, Lena Oberdorf, 20, alitawazwa Chipukizi Bora naye fowadi Beth Mead wa Uingereza akaibuka Mchezaji Bora na Mfungaji Bora wa makala ya Euro mwaka huu.

Ingawa Mead, 27, alipachika wavuni mabao sita sawa na Alexandra Popp wa Ujerumani, alizoa kiatu cha dhahabu kutokana na wingi wa krosi na pasi zilizozalisha mabao (tano). Nyota huyo wa Arsenal alicheka na nyavu za wapinzani katika mechi nne kati ya sita, yakiwemo magoli matatu (hat-trick) dhidi ya Norway katika mechi ya hatua ya makundi mnamo Julai 11.

Popp, 31, alifunga katika mechi tano zilizosakatwa na Ujerumani kabla ya fainali, yakiwemo mabao yote mawili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Ufaransa katika nusu-fainali.

“Huu ni wakati wa sherehe. Tulistahili kupata ushindi huu wa kihistoria kwa sababu tuna kikosi kizuri kinachocheza kwa kujituma. Ndoto yetu ya kwanza imetia, sasa tunalenga kutamalaki fainali za Kombe la Dunia zitakazoandaliwa mwakani nchini Australia na New Zealand,” akasema Wiegman.

Fainali ya Jumapili ilikuwa ya tatu kwa Uingereza kunogesha kwenye kipute cha Euro. Warembo hao walifunga mabao 22 huku wapinzani wakitikisa nyavu zao mara mbili. Walifungua kampeni za Kundi A kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Austria kabla ya kudhalilisha Norway 8-0 na kukomoa Northern Ireland 5-0. Walipepeta Uhispania 2-1 kwenye robo-fainali kabla ya kudengua Uswidi kwa kichapo cha 4-0 katika hatua ya nne-bora.

Ushindi wa Jumapili uliwafanya kuwa kikosi cha tano tofauti baada ya Ujerumani, Uswidi, Norway na Uholanzi kuwahi kutamalaki kivumbi cha Euro kwa upande wa wanawake. Mbali na kuzoa taji mbele ya mashabiki wao wa nyumbani, Uingereza walilipiza kisasi dhidi ya Ujerumani waliowatandika 6-2 katika fainali ya Euro 2009 nchini Finland.

Ujerumani wanaonolewa na Martina Voss-Tecklenburg, ndicho kikosi kinachojivunia mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Euro za wanawake. Wamenyanyua taji la Euro mara nane kutokana na makala 12 yaliyopita.

Walitawazwa malkia wa Euro mara sita mfululizo kati ya 1995 na 2013 huku jaribio lao la kutwaa ubingwa kwa mara ya saba mfululizo likizimwa na Denmark kwa kichapo cha 2-1 katika hatua ya robo-fainali mnamo 2017 nchini Uholanzi.

Walianza kampeni zao za Kundi B kwa ushindi wa 4-0 dhidi ya Denmark kabla ya kucharaza Uhispania 2-0 na kukung’uta Finland 3-0. Matokeo hayo yaliwapa motisha ya kubandua Austria kwa mabao 2-0 katika hatua ya nane-bora kabla ya kupiga miamba Ufaransa 2-1 katika nusu-fainali. Bao dhidi ya Ufaransa lilikuwa lao la kwanza kufungwa kwenye Euro mwaka huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Warembo wa Brazil wazamisha Colombia na kutawazwa malkia wa...

Mwendeshaji bodaboda afariki katika ajali Kirinyaga

T L