Vipusa wa Uingereza waweka rekodi mpya ya ufungaji mabao baada ya kuponda Latvia 20-0

Vipusa wa Uingereza waweka rekodi mpya ya ufungaji mabao baada ya kuponda Latvia 20-0

Na MASHIRIKA

KIPUSA Ellen White aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Uingereza baada ya kuongoza kikosi chao kupepeta Latvia 20-0 mnamo Novemba 30, 2021.

White, 32, alivunja rekodi ya Kelly Smith ya mabao 46 huku magoli yake matatu yakifikisha rekodi yake ya magoli hadi 48 kutokana na mechi 101 ndani ya jezi za Uingereza.

Fowadi huyo wa Manchester City alihitaji dakika tisa pekee uwanjani kuvunja rekodi ya Kelly huku mwenzake mwingine wa Man-City, Lauren Hemp akitikisa nyavu mara nne uwanjani Keepmoat. Beth Mead wa Arsenal na Alessia Russo wa Manchester United walifunga mabao matatu kila mmoja.

Mechi hiyo ilimpa Jess Carter jukwaa la kufunga bao lake la kwanza kimataifa, Katie Zelem wa Man-United aliwajibikia Uingereza kwa mara ya kwanza huku beki Millie Bright akivalia utepe wa unahodha kwa mara ya kwanza.

Kulikuwa na wafungaji 10 katika mechi hiyo iliyoshuhudia pia Ella Toone, Georgia Stanway, Bethany England, Jill Scott na Jordan Nobbs wakicheka na nyavu za Latvia.

Uingereza wanasalia kileleni mwa kundi lao la kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia baada ya kushinda mechi zote sita zilizopita ambazo zimewavunia mabao 53 bila ya wapinzani kutikiswa na wapinzani.

Ushindi wao wa 20-0 ulivunja rekodi yao ya awali ya 13-0 dhidi ya Hungary mnamo 2005. Latvia walishuka dimbani kuvaana na Uingereza mjini Doncaster wakiwa na matumaini machache baada ya kikosi hicho kuwanyanyasa 10-0 mnamo Oktoba 2021.

Wafungaji Bora wa Muda Wote katika timu ya wanawake ya Uingereza:

48 – Ellen White

46 – Kelly Smith

44 – Kerry Davis

40 – Karen Walker, Fara Williams

35 – Hope Powell

33 – Eni Aluko

32 – Karen Carney

30 – Gillian Coultard

28 – Marieanne Spacey

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

CECIL ODONGO: Kina mama wajitokeze na kusaka kura bila...

Msiwape sikio wanaofanya siasa za ukabila, Gavana Mvurya...

T L