Dondoo

Vipusa wahamia kwa polo mkora

December 11th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

NETIMA, BUNGOMA

POLO mmoja kutoka eneo hili alijipata taabani baada ya warembo wawili kumvamia wakitaka awaoe wote.

Inadaiwa warembo hao waliudhika sana walipogundua kuwa polo anawachezea shere akichovya asali ya kila mmoja kisiri.

Kulingana na mdokezi, mabanati hao walipata fununu kutoka kwa wenyeji kuhusu mienendo ya polo, na alivyokuwa akiwacheza kimapenzi.

Kutia msumari moto kwenye kidonda, vipusa hao walikuwa wakijuana kwani walisomea shule moja ya msingi licha yao kuishi vijiji tofauti.

Duru zinasema walisikizana kumuwekea polo mtego.

Siku ya tukio, polo alimpigia mrembo mmoja simu aende kumhudumia kama ilivyokuwa desturi.

Punde tu mrembo huyo akamjuza mwenzake na wakaamua kukutana kwa polo.

Walipofika nyumbani kwa jamaa kila mmoja alikuwa amebeba mkoba ulioonekana kuwa na nguo mke ndani.

“Tumekuja utuoe sote sasa. Hakuna haja ya wewe kula kwangu kisha unapagusa mdomo kama paka na kumrukia mwenzangu pia,” kipusa mmoja alifoka.

Habari zilizotufikia zinasema kuwa jamaa alimaka na kubaki mdomo wazi.

“Hakuna pahali tunaenda. Kuanzia leo tumekubali kuwa wake wenza. Tumekuletea asali karibu, tena mizinga yote miwili,” mabinti hao walimkaripia polo.

Waliendelea: “Hatubanduki sisi. Umekuwa na mazoea ya kutoka kwangu unaenda kwake. Ukitoka kwake unakuja kwangu. Leo unatuoa sote wawili!”

Kalameni alijaribu kuwarai warudi kwao ili kwanza ajipange, lakini vidosho hao wenye hasira hawakutaka kusikia lolote.

“Umekuwa ukitupiga mashuti papa hapa ndani ya hii nyumba, jinsi ilivyo. Hakuna kujipanga. Tutaishi na wewe hapa,” polo aliambiwa.

Duru zinasema polo aliamua kutorokea kwa mamake mambo yalipomzidia, akajifungia humo.

“Anafikiri sisi ni wajinga. Hatuondoki hapa. Tabia zake tunazijua. Hata pengine kuna wengine kadhaa kule nje,” mrembo mmoja alidai.