Dondoo

Vipusa walimana kanisani wakizozania polo

September 5th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

Kibabii, Bungoma

Waumini wa kanisa moja la hapa walibahatika kutazama sinema ya bure mrembo mmoja alipomuangushia mwenzake makofi kanisani akimlaumu kwa kueneza umbea kumhusu.

Inadaiwa mrembo alikasirishwa na madai ya mwenzake kwamba alikuwa akimtongoza mumewe.

Kulingana na mdokezi, purukushani hizi zilianza pindi tu pasta alipotamatisha ibada.

Duru zinasema mrembo alimkaribia kipusa na kumtaka afafanue madai aliyoibua.

“Nimesikia unatangatanga kila mahali ukinichafulia jina. Hebu nieleze bwanako nilimtongoza lini na ana nini spesheli ninachoweza kutaka wake?” mrembo alimfokea kipusa.

Kipusa alimuangalia mrembo yule usoni na kumuonya asidhubutu kuzungumza na bwana yake tena.

“Kila mtu anakujua. Tafuta mume wako. Wewe hujui vile nilihangaika nikitafuta mzee. Mwizi wewe!” alimuonya mrembo.

Penyenye zinasema mrembo alinyoosha mkono na kumpa kipusa makofi mawili makali.

“Naona umenizoea. Utakoma kucheza na mkia wa mamba,” alimuonya kipusa huku milio ya makofi ikisikika.

Waumini wa kanisa waliokuwa karibu waliingilia kati kuwatenganisha.

“Eti mimi namtafuta bwana yake. Wewe ukiangalia ananiweza kweli,” mrembo alimkaripia kipusa. Vicheko vilisikika kwote. “Una bahati. Kama si hawa, ningekugonga mpaka ushangae,” mrembo alifoka.

Mrembo aliamua kuondoka. “Ukiniletea ujinga tena mimi nitakupondaponda. Sikuogopi,” alimuonya kipusa huku akienda.

Kila mtu alibaki mdomo wazi. Iliwabidi Waumini kumuita pasta ili aweze kuwapatanisha wawili hawa.

Ilisemekana kuwa kipusa alikuwa amepata fununu kwamba mwanadada huyo alikuwa akimmezea mate mumewe na walikuwa wameonekana pembeni.

Hata hivyo hakukuwa na ushahidi kwamba walishiriki ufuska. Pasta wa kanisa hilo aliahidi kuzungumza na wawili hao kutatua mzozo huo.