Dondoo

Vipusa wazua kioja baa wakizozania bia ya polo

January 9th, 2019 1 min read

Na LUDOVICK MBOGHOLI

MOMBASA MJINI

Mabinti wawili walizua kioja kwenye baa moja katikati ya jiji hili wakizozania pombe waliyonunuliwa na kalameni.

Kisanga hicho kiliwashangaza wateja waliokuwa ndani ya baa hiyo wakiburudika.

Mdokezi anatupasha kwamba mabinti hao walitambua jamaa huyo alikuwa mwepesi wa kuwastarehesha warembo na wakamkaribia wajuane huku wakimzingua kwa tabasamu ili wamuingize ‘boksi’ mzimamzima.

Bila kujitambua jamaa aliwaambia wavute viti waketi karibu naye wajienjoy, nao mabinti wakasongea wakimpa tabasamu.

Jamaa alianza kuwarushia mistari. “Nimekuwa nikiwaona lakini niliogopa kuwakaribia,” aliwaambia nao hawakusita kumjibu. “Tumekuwa tukikufeel lakini tulishindwa tutaanzaje maana wanaume ni moto wa kuotea mbali,” mmoja alisema.

Kulingana na mdokezi, jamaa alimwagiza weita kuwapa pombe na mabinti wakaitisha vinywaji walivyopenda.

“Waliagiza pombe ya bei ghali sana naye jamaa akachomoa kipochi chake na kulipia kila mmoja chupa sita sita,” alisema mdokezi.

Vinywaji vilipoletwa mabinti walivivamia kwa fujo na baada ya saa moja chupa zilikuwa tupu na akaambia weita achafue meza tena.

Usiku ulipoingia, mabinti walikuwa wamelewa na wakaanza kubishania jamaa huyo kila mmoja akidai alikuwa mtu wake.

“Vurugu zilizidi walipoanza kung’ang’ania pombe kila mmoja akidai chupa zilizokuwa mezani zilikuwa zake. Malumbano yalizidi na kujenga uadui kati yao,” alisema mdokezi.

Juhudi za jamaa kuwatuliza hazikufua dafu huku kelele zao zikitanda ndani ya baa. “Jameni mnagombania nini na mimi ndiye nimenunua pombe,” jamaa aliwaambia huku wakimpuuza na kuendelea kuvutana.

Inasemekana jamaa alilazimika kuondoka kimyakimya na walinzi wakaja kuwafurusha wawili hao kwa kuvuruga amani kwenye kilabu hicho.