Dondoo

Vipusa wazua vurugu hotelini wakizozania ndume

Na JOHN MUSYOKI August 29th, 2024 1 min read

Kithimani, Yatta

KIOJA kilizuka kwenye soko moja mtaani hapa baada ya kina dada wawili kuzua fujo mmoja wao akimlaumu mwenzake kwa kumpokonya mpenzi wake.

Mwanadada wa kwanza alijitoma kwenye hoteli moja huku akihema kwa hasira na kumkabili mwenzake aliyekuwa akila nyama ya kuku na chips.

Alimnyanyua kipusa kutoka kitini na kumwaga chakula chake.

“Kwa nini unajaribu kushindana na mimi? Umeniharibia uhusiano kwa tamaa zako. Wachana na mpenzi wangu ama nikuharibu sura. Sitakubali uninyang’anye mpenzi wangu,” demu alimfokea mwenzake.

Mwanadada huyo alidai mpenzi wake ndiye alikuwa amempatia demu huyo pesa za kununua kuku kwenye hoteli hiyo.

Ilibidi wawili hao kutimuliwa hotelini walipoanza kukosesha wateja wengine amani.