Habari

Visa vya maambukizi ya Covid-19 vyagonga 700

May 11th, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

KENYA imethibitisha Jumatatu visa 28 vipya vya Covid-19 ambavyo kimaeneo ni Mombasa (10), Kajiado (9), Nairobi (7), na Wajir (2); na hivyo kufikisha 700 idadi jumla tangu kisa cha kwanza kilipogunduliwa mnamo Machi 13, 2020.

Visa hivyo vipya vimegunduliwa baada ya sampuli 840 kupimwa ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi, Waziri Msaidizi Rashid Aman amesema idadi jumla ya wale ambao wamapona kufikia sasa imefika 251 baada ya wagonjwa 12 zaidi kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Na katika kisa cha kuhuzunisha Dkt Aman ametangaza kifo cha mgonjwa mmoja kutoka Kaunti ya Nairobi na hivyo kuongeza idadi ya waliofariki kufika wahanga 33.

Wagonjwa wapya tisa kutoka Kajiado ni Wakenya na ni madereva ambao walikuwa wakirejea kutoka Tanzania.

Walipimwa katika mji wa mpakani wa Namanga.

Akielezea taharuki kuhusu ongezeko la maambukizi Kajiado Dkt Aman amesema ni sharti raia wawe makini na kuisaidia serikali.

“Tukome kuleta ugonjwa huu kutoka taifa jirani. Tunahimiza jamii zinazoishi mpakani ziwe macho na kuripoti wanaoingia nchini bila kufuata sheria tulizoweka,” Dkt Aman akasema.

Waziri huyo msaidizi pia amesema madereva watano raia wa Tanzania walipatikana na Covid-19 hivyo wakazuiwa kuingia nchini na akafafanua kwamba serikali ya Kenya imewasiliana na ya taifa hilo serikali yao iwashughulikie.

“Ninashauri kila mmoja awe ndugu mlinzi wa mwenzake. Tukishirikiana tutashinda Covid-19,” akasema.

Dkt Aman amebainisha kwamba kufikia sasa jumla ya kaunti 19 zimeathirika na virusi vya corona.

“Sasa ni wazi kuwa virusi hivi vinasambaa kote nchini. Tunapoingia katika mwezi wa tatu, kila mmoja awe mlinzi wa mwenzake,” akasema akiongeza kuwa azma kuu ya serikali sasa ni kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo katika jamii.

Dkt Aman amewahimiza Wakenya kuripoti katika vituo vya afya vya karibu endapo watahisi kuwa na dalili za ugonjwa wowote ule.

“Tunataka kuwajimiza Wakenya kutoogopa hospitali kwani vituo hivyo vya afya ni salama. Kila mmoja yuko huru kufika katika hospitali yoyote na kusaka huduma yoyote ya kimatibabu,” akasema.

Serikali pia imezindua nambari za dharura za mtandao wa WhatsApp, unaolenga kuimarisha kampeni dhidi ya janga la corona nchini.

“Tumezindua nambari 0110719719 kwa ajili ya mawasiliano ya WhatsApp; hivyo watu watumie kupasha ujumbe na pia kupata ushauri,” Dkt Aman akaeleza.

Dkt Aman amesema serikali inaendelea kujadiliana uwezekano wa kufunga mpaka wa Namanga, unaounganisha Kenya na Tanzania.