Michezo

Visa vya mastaa wa EPL kuvamiwa vyaongezeka

June 12th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

POLISI wanaochunguza kisa cha uvamizi na wizi wa fedha na bidhaa zenye thamani ya Sh70 milioni katika nyumba ya fowadi wa Manchester City, Riyad Mahrez, 29, wamemtia nguvuni mshukiwa mmoja.

Maafisa wa polisi wa Kituo cha Greater Manchester nchini Uingereza wamesema wamemkamata mwanamume mmoja wa umri wa miaka 28 anayetuhumiwa kushirikiana na majambazi kuvamia makazi ya Mahrez jijini Manchester.

Kamera za CCTV zilizonasa baadhi ya matukio hayo, zinaonyesha wanaume wanne wakitumia funguo za kujitengenezea wakiingia nyumbani kwa Mahrez na kupekua vyumba vitano vya kasri lake pindi baada ya sogora huyo mzawa wa Algeria kuondoka.

Polisi wameelezea ugumu wa kutambua sura za majambazi hao waliokuwa wamefunika nyuso zao kwa vitambaa.

Mbali na kutwaa Sh7 milioni pesa taslimu na jezi za soka zenye thamani ya Sh21 milioni, majambazi hao walihepa pia na saa za thamani kubwa, zikiwemo Mille ya Sh32.2 milioni, Rolex Daytona ya Sh5.6 milioni na Rolex Day-Date ya Sh4.9 milioni.

Kukamatwa kwa mshukiwa mmoja wa wizi huo unatokea siku moja baada ya beki wa zamani wa Manchester United, David May, 49, pia kuvamiwa nyumbani kwake katika eneo la Chadderton, Manchester na majambazi watatu waliomwibia gari aina ya Audi S4 lenye thamani ya Sh6.3 milioni.

Mahrez ndiye mwanasoka wa hivi karibuni zaidi baada ya Dele Alli na Jan Vertonghen wa Tottenham Hotspur na Mamadou Sakho wa Crystal Palace kuvamiwa na wahalifu nyumbani kwao.

Alli aliachwa akiuguza majeraha ya uso baada ya kuvamiwa na majambazi usiku wa kuamkia Mei 14 nyumbani kwake jijini London, Uingereza.

Majambazi wawili waliokuwa na visu vyenye makali walivunja mlango wa mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 24 ambaye kwa sasa anaishi na kakaye mdogo na wachumba wao.

Alli pia alitishiwa maisha na kupigwa magumi kadhaa usoni wakati wa uvamizi huo.

Wavamizi walifaulu kuponyoka na mapambo ya dhahabu na saa za mkononi zenye thamani kubwa. Kisa hicho kingali kinachunguzwa baada ya Alli kuwasilishia polisi video ya CCTV iliyonasa tukio hilo.

Mnamo Machi, 2020, familia ya Vertonghen ilivamiwa na majambazi na kuibiwa pesa na bidhaa za thamani isiyojulikana wakati sogora huyo alipokuwa uwanjani akiwasakatia waajiri wake kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Mnamo Februari 2019, genge la majambazi lilivamia makazi ya fowadi wa Liverpool na timu ya taifa ya Senegal, Sadio Mane na kuiba saa, simu na funguo za gari.

Mwezi mmoja kabla, Dane ambaye ni kakaye mfumaji Marcus Rashford wa Manchester United na Tyler ambaye ni kakaye beki Trent Alexander-Arnold wa Liverpool pia walivamiwa kwa pamoja na majambazi sita katika mkahawa mmoja jijini Manchester na kuibiwa saa za thamani ya Sh3.5 milioni na magari ya Sh42 milioni.

Mnamo 2017, Andy Carroll alifuatwa na majambazi wawili waliokuwa kwenye pikipiki alipokuwa akiliendesha gari lake kuelekea nyumbani baada ya kushiriki mazoezi katika uwanja wa London unaomilikiwa na kikosi cha West Ham United. Walifaulu kumwahi na wakamwibia saa aina ya Rolex yenye thamani ya Sh3 milioni.

Aliyekuwa kiungo na nahodha wa Uingereza na Man-United, Wayne Rooney aliwahi pia kuvamiwa na majambazi nyumbani kwake Cheshire, Uingereza na kumwibia Sh560 milioni pesa taslimu mnamo 2016 kabla ya wahalifu hao kumshambulia fowadi wa zamani wa Everton, Romelu Lukaku wa Inter Milan.