Habari Mseto

Visa vya mauaji ya abiria wa teksi vyazua wasiwasi

February 6th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MAUAJI ya Mildred Odira, mfanyakazi wa kampuni ya Foresight Innovations aliyekuwa akifanya kazi katika shirika la Nation Media Group yamefanya Wakenya kuhofia usalama wao wakisafiri kwa teksi.

Mildred alitoweka baada ya kuondoka kwake usiku kwa teksi kwenda hospitali kabla ya mwili wake kupatikana katika mochari wiki moja baadaye.

Rekodi za polisi zinaonyesha kuwa visa vya madereva wa teksi kuhusishwa na mauaji au utekaji nyara wa wateja wao vimekuwa vikiripotiwa nchini hasa jijini Nairobi.

Kuuawa kwa Mildred kulijiri polisi wakiendelea na uchunguzi kubaini iwapo waliomuua Bi Mary Wambui Kori ambaye mwili wake ulipatikana eneo la Ruiru walitumia huduma za teksi kwenda kuutupa.

Inashukiwa kuwa Bi Wambui aliuawa katika nyumba ya mpenzi wa mumewe eneo la Kiambu kabla ya mwili wake kusafirishwa kwenda kutupwa.

Mnamo Oktoba mwaka jana, mwanamke kwa jina Wandera alisimulia masaibu yake mikononi mwa dereva wa teksi aliyetaka kumteka nyara.

Mwanamke huyo alisema dereva huyo alikataa kufungua milango yake alipofika alikokuwa akienda na kuwapigia simu watu wengine akidai alikuwa amekataa kulipa nauli.

“Alinipitisha nilikokuwa nikienda kwa takriban kilomita moja bila maelezo. Nilipomuuliza alidai nilikuwa nikimsumbua kisha akapigia simu watu wengine kuwaarifu kwamba kuna mteja aliyekuwa akimsumbua. Watu wawe waangalifu wanapotumia huduma za teksi,” alieleza mwanamke huyo kwenye ujumbe alioandika katika mitandao ya kijamii.

Mwaka jana pia, mwanamke kwa Sheilla Mkenya alieleza mtandaoni alivyonusurika kubakwa na dereva wa teksi mtaani Buruburu.

“Ni kwa bahati niliokolewa na walinzi,” alieleza.

Mnamo 2017, dereva wa teksi kwa jina Anthony Kanyari alishtakiwa katika mahakama ya Milimani kwa kumbaka mwanamke mteja wake. Ilidaiwa kwamba mwanamke huyo alipanda teksi yake kutoka eneo la Ngara, Nairobi alfajiri ya Julai 31 2017 kabla ya mshtakiwa kuungana na watu wengine kumdhulumu kimapenzi.

Kushtakiwa kwa dereva huyo kulifuata kisa kingine ambapo Bw Zacharia Gachecha, dereva mwingine wa teksi jijini Nairobi alishtakiwa kwa kushirikiana na watu wengine kumteka nyara raia wa Burundi kutoka mkahawa mmoja kwenye barabara ya Ngong.

Katika kisa kingine Kaunti ya Embu, polisi eneo la Manyatta walimkamata dereva wa teksi aliyedaiwa kumbaka mwanamke aliyekuwa na umri wa miaka 31.

Ilidaiwa kwamba, dereva huyo na mtu mwingine walimpeleka mwanamke huyo hadi eneo la Kibugu kutoka mji wa Embu walipombaka kwa zamu wakitisha kumuua.

Madereva wa teksi pia wamekuwa wakitekwa nyara na hata kuuawa na majambazi wanaojifanya wateja.

Mnamo 2016, Joseph Muiruri aliyekuwa dereva wa teksi aliuawa pamoja na mteja wake wakili Willy Kimani na Josphat Mwenda walipotekwa nyara wakitoka katika mahakama ya Athi River.