Habari

Visa vya wananchi kuwapiga polisi vyaibua wasiwasi tele

May 11th, 2020 2 min read

Na WAANDSHI WETU

MTINDO ambapo wananchi wameanza kuchukua sheria mikononi mwao na kuwashambulia polisi unaibua hofu nchini.

Hili linatokana visa kadhaa wiki jana ambapo wananchi wameghadhabika na kuwageukia polisi kwa hasira.

Mnamo Jumatano wiki jana, wananchi wenye ghadhabu walimpiga mawe polisi katika Kaunti ya Homa Bay, kwenye kisa ambacho kimewashangaza wakazi wengi wa eneo la Nyanza.

Mwathiriwa alitambuliwa kama Bw Felix Yegon, ambapo alishambuliwa jioni na wenyeji wa kijiji cha Kalwal, katika kata ndogo ya Kasirime Kawanga.

Alikuwa ameandamana na mwanamume ambaye alikuwa akijaribu kumchukua mkewe kutoka kwa mwanamume mwingine aliyekuwa akitaka kumrithi.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Ndhiwa, Bw Robert Aboki, alisema kuwa marehemu alikuwa kazini wakati mkasa huo ulipotokea.

Alikuwa akihudumu katika Kituo Kidogo cha Polisi cha Kobama, kilicho katika eneo hilo. Alisema kwamba alikuwa na polisi mwenzake na mwanamume aliyetaka kumrejesha mkewe.

Hata hivyo, wakazi walisema kuwa marehemu alikuwa ameandamana na mhalifu anayejulikana sana katika eneo hilo ndipo wakamshambulia.

Katika mji wa Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua, polisi mmoja mwanamke alipata majeraha mabaya mnamo Jumatano baada ya kupigwa mawe na wakazi wenye ghadhabu.

Mwathiriwa alikuwa miongoni mwa polisi kadhaa ambao walikuwa wakifanya msako dhidi ya wenye baa ambao bado wanauza pombe licha ya marufuku ambayo yametolewa na serikali.

Wakazi waliwageukia polisi hao huku wakiwalaumu kwa kushirikiana na kuwalinda baadhi ya wenye baa, ambao bado wanaendelea kuuza vileo hivyo licha ya marufuku hayo.

Polisi hao walifika katika mojawapo ya baa mjini humo, ambayo iko karibu na Afisi ya Naibu Kamishna wa Kaunti Ndogo ya Ol Kalou ya Kati kuwakamata watu waliokuwa wakiendelea kunywa pombe.

Hilo lilifuatia malalamishi yaliyotolewa na baadhi ya wakazi kuhusu kelele ambazo watu hao walikuwa wakitoa.

Walipofika katika baa hiyo, walichukua muda mrefu kabla ya kuwakamata watu hao, hali iliyoufanya umati wenye ghadhabu kuwashambulia. Watu hao walidai polisi walikuwa wakijifanya bila kuwachukulia hatua.

Katika Kaunti ya Bomet, polisi watatu na mtu mmoja wanauguza majeraha baada ya kupata kichapo kikali kutoka kwa wananchi waliodaiwa kuwahangaisha na kuwaitisha pesa. Kisa hicho kilifanyika katika Kituo cha Kibiashara cha Ndanai, eneobunge la Sotik mnamo Jumamosi jioni.

Polisi watatu wa akiba walilazimika kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya wananchi wenye ghadhabu waliotaka kuwachoma.

Katika Kaunti ya Kakamega, diwani mmoja aliungana na vijana kadhaa Aprili na kuwakamata polisi wawili waliodaiwa kuwahangaisha wananchi kwa kuitisha hongo kutoka kwa watengenezaji chang’aa katika Kaunti Ndogo ya Navakholo.

 

Ripoti za George Odiwuor, Waikwa Maina, Vitalis Kimutai na Shaban Makokha