Kimataifa

Visa vya wanaume kujifyatua risasi nyeti kimakosa vyazidi

May 15th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU
 
MWANAMUME kutoka Nebraska, US amelazwa hospitalini baada ya kujipiga risasi sehemu nyeti kwa bahati mbaya.
 
Peter Jacobsson mwenye umri wa miaka 32 aliripotiwa kuwa Jumatano jioni alijipiga risasi kimakosa, wakati bunduki aliyokuwa ameweka mfukoni ilianguka sakafuni, na kujipiga risasi.
 
Tukio hilo lilipotokea, Jacobsson alikimbizwa katika hospitali ya Bryan West, japo hakupata majeraha mabaya.
 
Licha ya kujijeruhi, polisi Alhamisi walimfungulia mashtaka ya kutoa silaha jijini na kumiliki silaha bila idhini.
 
Si mara ya kwanza kwa mwanamume kujipiga risasi kimakosa katika sehemu nyeti kwani mnamo Februari, mwanamume mwingine wa miaka 46 kutoka Indiana alijifyatua risasi katika uume kwa bahati mbaya.
 
Mwanamume huyo alikuwa ameweka bunduki hiyo kwenye mshipi kiunoni, bila kifaa cha kuishikilia. Polisi walisema alisikia ikiteremka, lakini alipopeleka mkono kuisongesha vyema ikamfyatukia.
 
Eneo la Arizona, mwanamume alijifyatua nyeti alipokuwa akisoma gazeti. Mwanamume huyo pia alikuwa ameweka bunduki yake kiunoni na ikaanza kuteremka ndipo akaifikia kuiweka sawa, lakini ikafyatuka.