Visa vya wizi wa mifugo vyazidi katika kijiji cha Maguguni Thika Mashariki

Visa vya wizi wa mifugo vyazidi katika kijiji cha Maguguni Thika Mashariki

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Maguguni, Thika Mashariki wanakadiria hasara baada ya mifugo wao kubwa na watu wasiojulikana.

Wakazi hao wanadai ya kwamba katika muda wa siku tatu zilizopita wamepoteza ng’ombe wanne na mbuzi wanane.

Bw Muiruri Kigera anaeleza kuwa kwa muda wa mwaka mmoja sasa wamepoteza mbuzi 100 na ng’ombe 15.

Alisema ya kwamba mnamo mwezi Januari wezi kadha waliovamia boma lake na alipojaribu kuwazuia wasiibe mifugo hiyo alikatwa kwa panga na kumjeruhi mkono wake wa kushoto.

Alisema wanashuku kuna watu wachache miongoni mwao ambao huenda wanashirikiana na wezi hao ambao hadi wa leo hawajakamatwa.

Licha ya kupiga ripoti kwa polisi hakuna hatua ambayo imechukuliwa ya kuwanasa wezi hao.

Kutokana na matukio hayo wakazi hao pia wanahofia maisha yao kwani wezi hao huwa wamejihami kwa mapanga, shoka na vyuma.

” Tunaiomba serikali ifanye hima kuona ya kwamba wahalifu hao wanakamatwa na kushtakiwa haraka iwezekanavyo,” alisema Bw Kigera.

Bi Mary Muthoni ambaye ni mjane anasema mnamo Ijumaa wiki jana alipoteza ng’ombe wake wanne.

“Sasa nimeachwa bila chochote na kwa hivyo ningeomba serikali inifikirie. Wakazi wengine wanaweka mifugo yao ndani ya nyumba zao wakiogopa kuwaacha walale zizini,” alisema Bi Muthoni.

Wakazi hao wanalaumu kitengo cha usalama kwa kukosa kuchukua hatua ya haraka kuzuia uhalifu huo.

 

You can share this post!

Kocha Joachim Loew hatimaye kuagana na timu ya taifa ya...

Jinsi upanzi wa mianzi unavyowafaidi wakazi wa Muranga