Visa vya wizi wa pikipiki za bodaboda vyaongezeka Witeithie

Visa vya wizi wa pikipiki za bodaboda vyaongezeka Witeithie

Na LAWRENCE ONGARO

WIZI wa pikipiki za bodaboda, umezidi katika kijiji cha Witeithie kilichoko Juja, Kaunti ya Kiambu.

Wahudumu wa bodaboda kutoka eneo hilo wanataka serikali kupitia kitengo cha upelelezi kuingilia kati ili kuelewa ukweli wa mambo.

Wahudumu hao pia wanadai ya kwamba pikipiki zinazoibwa ni zile ambazo walichukua kwa mkopo wa malipo ya polepole.

Mwathiriwa Bw Jeff Kinyanjui anasema ya kwamba mnamo Jumatano, pikipiki yake iliibwa akiwa ameiegesha nje karibu na jumba fulani.

Hii ni licha ya kuwa na kifaa cha kufuatilia inapoibwa popote.

Kulingana naye, alinunua pikipiki kwa deni ambapo iligharimu Sh160,000 na akiwa na deni la Sh 20,000 ili akamilishe kulipia pikipiki hiyo.

Wahudumu wa bodaboda katika eneo la Witeithie sasa wanataka maafisa wafanye uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa mambo kwa sababu pikipiki zilizo na vidhibiti vya kunasa wezi ndizi zinazoibwa pekee.

Wanataka pia waliowauzia pikipiki zhizo wasaidie katika kuchunguza jambo hilo ili kupata ukweli wa mambo.

Bw Kinyanjui alisema vijana wengi wanaoendesha biashara ya bodaboda wameachwa na wasiwasi baada ya pikipiki kadha kuibwa kwa muda wa wiki chache zilizopita.

“Iwapo hatua ya haraka haitachukuliwa, bila shaka vijana wengi wanaotegemea bodaboda watakosa njia ya kujikimu kimaisha,” alisema Bw Kinyanjui.

Mwenyekiti wa wahudumu wa bodaboda eneo la Witeithie Bw Michael Ngari, alisema inatia shaka kwa sababu pikipiki zilizo na madeni ndizo zinazoibwa na kwa hivyo polisi wanastahili kuingilia kati ili kujua ukweli wa mambo.

Alisema maisha yamekuwa magumu kwa vijana wengi ambapo matukio ya aina hiyo yanaponza juhudi zao za kujiendeleza.

“Sisi wahudumu wa bodaboda tutaungana ili tuzungumze kwa sauti moja ili matakwa yetu yaweze kutatuliwa,” alisema Bw Ngari.

Walisema wangetaka serikali kuingilia kati haraka iwezekanavyo ili kuwaokoa kutokana na wizi huo.

“Tunahofia maisha yetu kwa sababu hatujui ni wakati upi pikipiki nyingine zitaibwa tunapoendelea na biashara zetu. Hata pengine tunashuku kuna kikundi cha watu kinaedesha uovu huo kwa minajili ya kuziuza pikipiki hizo kwa manufaa yao wenyewe,” alisema mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti huyo aliwashauri wanabodaboda hao kuwa watulivu huku uchunguzi ukiendelea ambapo pia aliwatahadharisha wawe macho wakati wowote wanapoendesha kazi hiyo na “kujua mteja wako ni nani.”

You can share this post!

Raia wa Zambia kumjua mshindi wa urais wikendi hii

Hatimaye msimu mpya wa EPL waanza leo