Vita baridi ndani ya Kenya Kwanza

Vita baridi ndani ya Kenya Kwanza

NA ONYANGO K’ONYANGO

VITA baridi vimeibuka ndani ya muungano wa Kenya Kwanza baina ya marafiki wapya wa Rais William Ruto na wale wa zamani.

Baadhi ya marafiki wa zamani wa Rais Ruto wananung’unika kuachwa katika teuzi mbalimbali zinazofanywa na Kiongozi wa Nchi serikalini.

Waliozungumza na Taifa Leo kwa siri Jumanne, walielezea jinsi walivyojitolea mhanga kupigania Dkt Ruto tangu 2018 lakini kufikia sasa hawajavuna matunda.

Kulingana na wao, wandani wapya wa Rais Ruto waliojiunga naye miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, ndio wamekuwa wakiteuliwa serikalini.

Japo wanaonekana kukerwa, wandani hao wa Rais Ruto wanahofia kujitokeza wazi kutoa vilio vyao.

Dkt Ruto amekuwa akiwatunuku viti waliotekeleza majukumu muhimu katika safari yake ya Ikulu.

Wanaolalamika wanadai kuwa Rais Ruto amekuwa akishauriwa visivyo na washauri wake kwa lengo la kuwasukuma pembeni baadhi ya wanasiasa ndani ya Kenya Kwanza.

“Baadhi ya washauri wa Rais wamekuwa wakimshawishi kuteua jamaa na marafiki zao na kutuacha sisi,” akasema mwanasiasa mwingine ambaye pia aliomba jina lake libanwe.

Hatua ya Rais Ruto kumtunuku aliyekuwa gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu kwa kumteua kuwa miongoni mwa makamishna tisa wa Tume ya Kusafisha Mito Jijini Nairobi, ni ithibati tosha kwamba Kiongozi wa Nchi amekuwa akirusha minofu kwa waliomsaidia kuendesha kampeni.

Wengine waliotunukiwa nyadhifa serikalini ni bwanyenye Humphrey Kariuki, mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza pombe, Africa Spirits Ltd na naibu mwenyekiti wa kamati ya kutatua mizozo ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) Bi Wambui Mungai aliyeteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano (CA).

“Nimekuwa nikipigania Dkt Ruto tangu 2018 na hata nilitumia rasilimali zangu katika kampeni. Lakini sijateuliwa kushikilia wadhifa wowote serikalini. Wengi wa waliotunukiwa nyadhifa waliungana na Rais mapema mwaka huu,” akasema kiongozi aliyeomba jina lake libanwe kwa kuhofia kusutwa na vigogo wa Kenya Kwanza.

Wandani wa Dkt Ruto wanaoamini kuwa waasisi wa chama cha UDA sasa wanategea nyadhifa za mawaziri wasaidizi (CAS).

“Nilituma maombi ya CAS, nataka kuvuna matunda ya kujitolea kwangu katika kupigania Dkt Ruto. Inavunja moyo kwamba walioungana nasi mwaka huu wanatunukiwa nyadhifa ilhali sisi hatuna kazi,” akasema.

Awali, Naibu Rais Rigathi Gachagua alikuwa amesema kuwa watu waliochelewa kujiunga na Kenya Kwanza hawatapewa nyadhifa serikalini.

Lakini Bw Gachagua alionya kuwa watu wangepewa nyadhifa kwa kuzingatia mchango wao katika ushindi wa Rais Ruto.

“Kuna walioshindwa katika mchujo na uongozi wa chama ukawasihi wasiwanie viti hivyo kama wawaniaji huru. Waliosikia wito huo na wakaacha kusimama watateuliwa serikalini na wasiwe na wasiwasi,” alisema Bw Gachagua mnamo Oktoba 19 alipokuwa katika eneo la Nandi Hills, Kaunti ya Nandi.

Watakaokosa kupata nyadhifa 23 za CAS au ubalozi itabidi wangojee zaidi nyadhifa katika mashirika ya umma na hata kandarasi za serikali.

Mwenyekiti wa UDA Johnson Muthama, hata hivyo, alipuuzilia mbali wanaolalamika huku akisema kuwa washirika wote wa Kenya Kwanza wako sawa bila kujali mtu aliingia lini.

“Nafasi za uwaziri zilikuwa 23 pekee ilhali Kenya ina kaunti 47 na muungano wa Kenya Kwanza una mamia ya wanasiasa wanaotegea nyadhifa,” akasema Bw Muthama.

Wakati wa hafla ya kuapisha makatibu 51 wa wizara Ijumaa, Rais Ruto alisema kuwa nyadhifa hizo hazikutolewa kwa familia, jamii au maeneo fulani ila kwa watu wanaofaa kutumikia Wakenya.

“Wanaolalamika ni wachoyo na wabinafsi hawana tofauti na baadhi ya wanasiasa walioteua watoto wao kushikilia nyadhifa fulani,” akasema Rais Ruto.

Mbunge wa Belgut Nelson Koech, ambaye ni mwandani wa Rais, anasema kuwa waliotunukiwa nyadhifa walitia saini mikataba na Dkt Ruto kabla ya kujiunga na Kenya Kwanza.

Kulingana na Bw Koech, wanasiasa wengi wa Kenya Kwanza ambao wangali katika ‘baridi ya kisiasa’ watanufaika na nyadhifa za CAS.

Mbunge wa Nyaribari Chache Zaheer Jhanda anasema kuwa Rais Ruto anafaa kupewa wakati ili kuamua viongozi watakaomsaidia kutimiza ajenda yake ya maendeleo kwa Wakenya.

Baadhi ya viongozi wa Kenya Kwanza wanaomezea mate nyadhifa za CAS ni Bw Muthama, aliyekuwa mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali, waziri wa zamani wa Michezo Rashid Echesa, aliyekuwa mbunge wa Soy Caleb Kositany, gavana wa zamani wa Migori Okoth Obado na aliyekuwa Seneta wa Kakamega senator Cleophas Malala.

Wengine ni aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko, mbunge wa zamani wa Kaunti ya Laikipia Cate Waruguru, aliyekuwa mbunge wa Starehe Margaret Wanjiru, naibu gavana wa zamani wa Kisii Joash Maangi, mbunge wa zamani wa Nairobi Millicent Omanga, mbunge wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Simon Mbugua, aliyekuwa mbunge wa Starehe Charles Njagua, aliyekuwa mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa kati ya wengineo.

  • Tags

You can share this post!

UFUGAJI: Ufugaji wa ndege aina ainati unavyompa kipato

TAHARIRI: Si busara serikali kurudisha ada za benki kwa...

T L