Vita vikali Afghanstan huku zaidi ya watu 40 wakiuawa

Vita vikali Afghanstan huku zaidi ya watu 40 wakiuawa

Na AFP

MAPIGANO makali yanaendelea kuchacha katika miji mikuu nchini Afghanistan, huku Umoja wa Mataifa (UN) ukisema kuwa, jumla ya watu 40 wameuawa kufikia sasa tangu Jumanne.

Mnamo Jumanne, watu 12 waliuawa kwenye shambulio lililofanywa na wanamgambo dhidi ya makazi ya Waziri wa Ulinzi, Bismillah Khan Mohammadi.

Kulingana na msemaji wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Wais Stanikzai, waliofariki walijumuisha wanamgambo wanne na raia wanane.

“Magaidi kadhaa walilipua gari wakilenga makazi ya Waziri wa Ulinzi Jumanne jioni. Hata hivyo, vikosi vya usalama vilifanikiwa kuwaua washambuliaji hao wanne baada ya saa kadhaa za ufyatulianaji risasi,” akasema.Miongoni mwa wale waliouawa ni mwanamke.

Watu 20 walijeruhiwa.Licha ya shambulio hilo, vikosi vya usalama vilisema hakuwepo nyumbani kwake wakati wa shambulio hilo.Msemaji wa Wizara ya Afya, Dastgir Nazari alisema, walichukua miili minane kutoka eneo la tukio huku watu 22 wakilazwa katika hospitali mbalimbali.

Kwenye ujumbe wake, waziri alikashifu shambulio hilo akisema, linaashiria hali ya uoga ambayo imewakumba wanamgambo hao.

“Hilo halitatamausha wala kuathiri juhudi za vikosi vyetu kukabili vitendo vya kigaidi nchini mwetu,” akasema.

Kufikia sasa, hakuna kundi ambalo limedai kuhusika kwenye shambulio hilo, ingawa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Amerika ilililaumu kundi la Taliban.

Saa chache baada ya shambulio, wakazi wa jiji la Kabul walijitokeza katika barabara za jiji hilo wakisema “Allahu Akbar!” (Mungu ni Mkubwa) kama njia ya kuliasi kundi hilo.

Matukio kama hayo yalishuhudiwa Jumatatu katika mji wa Herat, ambao pia umekuwa ukikumbwa na mapigano katika siku za hivi karibuni.

Mapigano vile vile yalishuhudiwa katika mji wa Lashkar Gah, ambao ni makao makuu ya mkoa wa Helmand.Kulingana na takwimu za UN, zaidi ya watu 40 wameuawa katika muda wa siku mbili pekee.

“Miili imetapakaa barabarani. Hatujui ikiwa waliouawa ni raia ama wanamgambo wa kundi la Taliban,” akasema mkazi mmoja ambaye hakutaja kutajwa.

“Mamia ya watu wametoroka makazi yao na kuelekea karibu na Mto Helmand,” akaongeza. Jeshi la taifa hilo liliwarai wenyeji kuondoka mji huo na kuelekea katika maeneo salama, linapojitayarisha kwa operesheni kali kuwafurusha wanamgambo hao.

Wanamgambo hao waliondolewa mamlakani na vikosi vya kijeshi vilivyoongozwa na Amerika miaka 20 iliyopita.Wanaripotiwa kudhibiti maeneo mengi katika taifa hilo.

You can share this post!

Akamatwa kwa kumfanyia mpenziwe mtihani

AKILIMALI: Mitishamba matibabu tosha kwa ng’ombe wake