Habari za Kitaifa

Vita vipya vyazuka kati ya Mwangaza na Naibu wake

January 25th, 2024 2 min read

NA DAVID MUCHUI

MGOGORO wa kisiasa katika Kaunti ya Meru umechipuka tena huku tofauti mpya zikidhihirika kati ya Gavana Kawira Mwangaza na naibu wake, Isaac Mutuma.

Mabishano baina ya mapasta hao wa zamani waliogeuka kuwa wanasiasa yameshuhudiwa tena na kuzua kumbukumbu ya kusambaratika kwa uhusiano wao wa kikazi Mei mwaka jana.

Mnamo Jumatano, wakazi walinasa gari la Naibu Gavana likiwa linasafirishwa kupelekwa Nairobi kufanyiwa ukarabati.

Wafuasi wa naibu huyo walidai kwamba gari hilo lilikuwa linapelekwa Nairobi kwa njama fiche ili kuhakikisha kwamba Bw Mutuma anakosa mbinu ya usafiri wa kuzuru maeneo kwa urahisi.

Soma Hisia mseto zaibuka baada ya Mwangaza kuokolewa na Seneti

Pia Mwangaza aanza kukwaruzana na madiwani tena

Hata hivyo, Katibu wa Kaunti ya Meru Kiambi Atheru aliambia Taifa Leo kwamba gari hilo la Naibu Gavana limekuwa likifanyiwa ukarabati katika eneo moja mjini Meru na kwamba lilikuwa linapelekwa Nairobi wa ukarabati wa ziada.

“Nasubiri ripoti ya Mkurugenzi wa Usimamizi wa Magari ili tuelewe kilichofanyika. Hata hivyo, sidhani kuna lolote la mno katika kupeleka gari Nairobi. Kuna magari mengine ya kaunti kwenye gereji Nairobi,” akasema Bw Atheru.

Hata hivyo, wakati wa tukio hilo lisilo la kawaida asubuhi, dereva alilazimishwa kupeleka gari hilo katika makazi rasmi ya Naibu Gavana.

Bw Mutuma alikubali kwamba gari hilo lilitwaliwa baada ya kushukiwa kuwa kwenye njama fiche.

“Gari lilipelekwa kwa gereji Desemba mwaka jana lakini nikaambiwa kwamba afisi ya gavana haikuidhinisha ununuzi wa vipuri. Kulikuwa na maagizo maalum kwamba hakuna pesa zozote zinastahili kulipia ukarabati wa gari langu rasmi. Kwa sababu ya kuchelewa huko, niliamua kulirekebisha kwa kutumia pesa zangu binafsi,” akasema Bw Mutuma.

Alisema alikuwa tayari kutafuta Sh310,000 zinazohitajika kurekebisha gari hilo mjini Meru.

“Niko tayari kutumia pesa zangu kwa sababu nimekuwa nikijiwekea mafuta tangu Juni ilhali ni gari rasmi la serikali. Lakini wakati gavana alipojua kwamba nilikuwa tayari kulirekebisha kwa hela zangu mwenyewe, maagizo yalitolewa kwa mkurugenzi wa usimamizi wa magari kulipeleka katika afisi za Toyota, Nairobi,” akasema.

Alidai kwamba Serikali ya Kaunti ina deni kubwa la kampuni hiyo ya magari, jambo lililofanya magari kadhaa kutwaliwa.

“Uamuzi wa kupeleka gari langu Nairobi ulinuia kuhakikisha kwamba gari hili linatwaliwa ili niwe sina mbinu ya usafiri. Inashangaza kwa sababu afisi ya Naibu Gavana haifai kutegemea maamuzi ya Gavana haswa kile nafaa kuwa nacho, ila ni jukumu la Tume ya Mishahara,” akasema.

Bw Mutuma anadai kwamba hii ni mojawapo ya mbinu zinazotumiwa na uongozi wa kaunti kumtishia tangu akosane na Gavana.

Mnamo Jumapili, Bw Mutuma alidai kwamba kumekuwa na njama za kumlazimisha ajiuzulu kutokana na uhusiano mbaya kati yake na mkubwa wake.

“Nimeambiwa nitapewa pesa nikijiuzulu kama Naibu Gavana. Lakini sikuchaguliwa ndio nilipwe kujiuzulu,” alisema.

Awali, Gavana Mwangaza alikiri kulikuwa na uhusiano baridi na naibu wake na kwamba hangeweza kumlazimisha kuridhiana.

Habari sawia Madiwani wa Meru wakerwa na hatua ya Gavana Mwangaza kutaka serikali ivunjwe

[email protected]