KimataifaMakala

Vita vya Iran na Trump vitakavyoathiri maisha ya Wakenya

January 9th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

WASIWASI umezuka nchini kuhusu uwezekano wa mzozo kati ya Iran na Amerika kuathiri hali ya maisha ya Wakenya.

Kwa mujibu wa wataalamu wa kiuchumi na usalama, kuna uwezekano mkubwa Kenya kuathirika baada ya utawala wa Rais Donald Trump kumwangamiza Luteni Jenerali Qasem Soleimani wa Iran wiki iliyopita.

Hii ni kwa sababu ya ushirikiano wa karibu kati ya Kenya na Amerika katika nyanja tofauti, na pia kutatizika kwa usafirishaji wa mafuta na uuzaji wa bidhaa za kilimo nchini Iran.

Soleimani alikuwa kamanda wa kijeshi Iran, na aliuawa kwa bomu la Amerika kwenye msafara wake katika uwanja wa ndege jijini Baghdad, Iraq.

Athari ya kwanza kuu inayotarajiwa ni ongezeko la bei ya mafuta, ambayo itaathiri bei ya bidhaa zingine vikiwemo vyakula.

Bei ya mafuta ulimwenguni ilipanda kwa asilimia mbili na huenda ikazidi kupanda kadri mzozo huo unavyoendela kuzorota.

Ukanda wa Mashariki ya Kati hutegemewa zaidi ulimwenguni kwa uzalishaji mafuta ndiposa kukiwa na vita eneo hilo, bei ya mafuta hupanda.

“Kwa upande wa Kenya, kuna uwezekano mkubwa bei ya mafuta itapanda na hii itaathiri uchumi wetu kama nchi na kibinafsi,” akasema Dkt Kemoli Sagala, ambaye ni mtafiti wa masuala ya utawala na mipango maalumu katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Sekta ya kilimo cha majani chai pia imeanza kuingiwa wasiwasi, kwani Iran ni mnunuzi mkubwa wa zao hilo kutoka Kenya.

Wahusika katika sekta hiyo jana walisema vitisho vya Iran kwamba italipiza kisasi kutokana na mauaji ya Soleimani huenda ikawatia hofu wafanyabiashara wanaouza majani chai ya Kenya nchini humo.

“Baadhi ya wafanyibiashara bila shaka watahofia kuuza majani chai katika masoko ya Iran kutokana na hofu ya kushambuliwa, na hii itaathri sana mauzo yetu,” akasema Bw Gideon Tuwei ambaye ni mtaalamu wa mauzo katika mnada wa majani chai.

Iran ilinunua kilo 532,715 za majani chai ya Kenya mwaka jana. Kenya huuza takriban asilimia 20 ya majani chai kwa taifa hilo la ukanda wa Mashariki ya Kati.

Vile vile, kutokana na kuwa Kenya ni mojawapo ya washirika wakubwa wa Marekani barani Afrika, kuna hatari ya kushambuliwa na makundi ya kigaidi yenye nia ya kulipiza kisasi kifo cha Soleimani, au makundi ya kigaidi yatakayojitafutia umaarufu kwa kujipendekeza kwa Iran.

Tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, usalama umeimarishwa jijini Nairobi hasa katika sehemu zinazotumiwa zaidi na raia wa kigeni.

Mfano ni katika Hoteli ya Hilton ambako kuna ulinzi mkali kutoka kikosi cha polisi cha GSU. Hoteli hiyo inamilikiwa na kampuni ya Hilton Worldwide Corporation iliyo na makao yake makuu Amerika.

Msemaji wa polisi, Bw Charles Owino alisema mashambulio ya kigaidi ya zamani yalidhihirisha Kenya imo hatarini kulengwa wakati mataifa mengine yanapoingia vitani.

“Tumeimarisha usalama kila mahali kwa sababu tuna historia ya mashambulio yanayolenga mataifa mengine,” akasema, na kuongeza kwamba uchunguzi utabainisha kama shambulio lililotokea katika uwanja mdogo wa ndege Manda, Kaunti ya Lamu mnamo Jumapili ulihusiana na mauaji ya Soleimani.

Mnamo 1998, Ubalozi wa Amerika nchini ulishambuliwa na magaidi wa kundi la al-Qaeda waliokuwa wakilipiza kisasi dhidi ya taifa hilo lenye ushawishi mkubwa ulimwenguni.

Taarifa ya Barnabas Bii, Mary Wambui, Aggery Mutambo na Valentine Obara