Vita vya ubabe kati ya gavana, Wetang’ula mazishini

Vita vya ubabe kati ya gavana, Wetang’ula mazishini

Na BRIAN OJAMAA

VITA vya ubabe kati ya Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati na Seneta Moses Wetang’ula viliendelea kushamiri mwishoni mwa wiki na kusababisha fujo mazishini.

Hii ni baada ya madiwani wanaomuungano mkono Gavana Wangamati kushambuliana vikali na na wale waaminifu kwa Bw Wetang’ula katika hafla ya mazishi ya Mama Selina Soita, mamake diwani wa zamani Patroba Soita katika kijiji cha Sitikho, Webuye.

Fujo zilianza wakati madiwani wandani wa Bw Wangamati walikashifu mwenzao wa wadi ya Sitikho, Grace Sundukwa kwa kuhujumu uongozi wa gavana huyo.

Walidai wenzao wanaoegemea mrengo wa mwenyekiti huyo wa Ford Kenya ndio wanaendesha kampeni za kumwezesha Spika wa Seneti Ken Lusaka kutwaa ugavana wa Bungoma katika uchaguzi mkuu ujao.

Madiwani hao; Bethwel Mwambu (wa wadi ya Mbakalu), David Barasa (Kimilili), Majani Mutoka (Maraka), Paul Wanyonyi (Matulo), Joruma Wanjala (Bukembe Mashariki), Violet Makhanu (Mihuu) miongoni mwa wengine badala yake walimshauri Bi Sundukwa kuungana na gavana Wangamati kufanikisha maendeleo katika kaunti hiyo.

Lakini fujo zilizuka diwani Sundukwa alipotwaa kipaza sauti kutoka kwa mwombolezaji mmoja na kuwashutumu wenzake kwa kumpotosha gavana huyo ambaye alihudhuria mazishi hayo.

“Bw Gavana, hawa madiwani wanaokufuata hawakuambii ukweli. Wanakupotosha. Wanafaa kujikita katika masuala yanayohusu wadi zao kwa manufaa ya wapiga kura wao,” akafoka diwani huyo wa chama cha Ford Kenya.

Bw Sundukwa ambaye anahudumu muhula wa kwanza kama diwani vile vile alimshutumu Naibu Gavana Charles Ngome kwa kutumia lugha chafu katika hafla za mazishi.

You can share this post!

Wabunge wamwekea mlipa kodi mzigo zaidi kwa kupendekeza...

Mrengo wa tatu wa kisiasa waibuka Bondeni