Habari Mseto

Vitabu milioni 32 kusambazwa shuleni muhula wa pili

April 2nd, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WACHAPISHAJI wanasema usambazaji wa vitabu vya kiada katika shule za umma chini ya mpango wa serikali wa kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi atatumia kitabu kimoja, utafanywa kabla ya shule kufunguliwa kwa muhula wa pili.

Chama cha Wachapishaji Vitabu Nchini (KPA) kiliambia seneti kwamba baadhi ya majukumu ambayo serikali ilizipa kampuni za uchapishaji vitabu zimezikamilisha na kazi iliyobaki itamalizika kabla ya Aprili 30, 2018.

Mpango huu mpya wa serikali kusambaza vita moja kwa moja shuleni umeiwezesha kuokoa Sh13.8 bilioni, pesa ambazo zilikuwa zikifyonzwa na wafanyabiashara walaghai ambao wamedhibiti sekta ya biashara ya vitabu nchini.

“Kufikia mwisho wa mwezi Aprili vitabu milioni 32.8 milioni vitakuwa vimewafikia jumla ya wanafunzi milioni tano wa darasa la Saba na Nane pamoja na wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi nne,” akasema mwenyekiti Lawrence Njagi.

Pia ilibainika kuwa usambazaji wa vitabu umecheleweshwa pia kutokana na hali kwamba ni kampuni moja tu miongoni mwa tano zilizopewa zabuni hiyo na serikali ina mitambo ya kupiga chapa.

“Wachapishaji wetu wote hawana mitambo ya kuchapisha vitabu isipokuwa kampuni ya Kenya Literature Bureau (KLB). Hii ina maana kuwa kampuni hizo zilikodisha huduma za uchapishaji kutoka kwa kampuni zingine,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kutayarisha Mitaala Nchini (KICD) Julius Jwan.

“Mnamo Januari mwaka huu, serikali ilisambaza vitabu 33 milioni za masomo ya kimsingi kama vile Kiingereza, Kiswahili, Hisabati, Bayolojia, Kemia, Fizikia katika shule za sekondari. Vitabu hivyo, viligharimu Sh7.5 milioni. Na wanafunzi wa madarasa ya saba na nane walipewa vitabu vya kiada vya masomo ya Kiingereza, Kiswahili, Hisabati na Sayansi,” akasema.