Habari

Vitabu vilivyopewa wanafunzi na Serikali vimejaa makosa – Walimu

March 6th, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

Kwa ufupi:

  • Walimu wasema walianza kugundua makosa mengi mara walipopewa vitabu hivyo, na sasa wamelazimika kuviweka kando
  • Tatizo hilo haliko kwa vitabu vya Kiswahili pekee bali pia katika vile vya masomo ya Kiingereza, Hesabu, Fizikia, Kemia na Bayolojia
  • KICD yalikiri kwamba kuna dosari katika baadhi ya vitabu na tayari kuna mikakati iliyowekwa kusahihisha makosa
  • Itaamuliwa baadaye kama vitabu husika vitahitaji kubadilishwa au walimu watafahamishwa kuhusu marekebisho yanayofaa kufanywa

WALIMU katika shule za umma za sekondari wameacha kutumia vitabu vilivyopewa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwezi Januari wakisema vinapotosha kutokana na makosa mengi.

Walimu waliohojiwa na Taifa Leo, ambao tumebana majina ili kuwalinda wasiadhibiwe, walisema walianza kugundua makosa mengi mara walipopewa vitabu hivyo, na sasa wamelazimika kuviweka kando. Walisema badala yake wanatumia vingine ili wasipotoshe wanafunzi wao.

Vitabu hivyo vilivyogharimu Sh7.5 bilioni vilipeanwa kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza chini ya mpango wa Elimu Bila Malipo. Usambazaji wa vitabu hivyo ulizinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi mnamo Januari 5 mwaka huu na kufikia sasa vimesambazwa kwa wanafunzi wa shule za umma.

 

Masomo yalioathirika

Malalamishi mengi zaidi yametoka kwa walimu wa Kiswahili ambao wanasema mojawapo ya vitabu walivyopewa kinaonekana kilichapishwa kwa haraka na kampuni moja mashuhuri ya uchapishaji nchini.

“Ni shida tupu. Tunakitumia tu kwa vile serikali ilisema tutumie lakini kina matatizo tele,” akasema mwalimu wa shule moja ya upili ya kitaifa.

Makosa yaliyopatikana katika baadhi ya vitabu vya Kiswahili ni kama vile mifano potovu ya vivumishi, nomino, vitenzi na utumizi wa vipengele ambavyo havitambuliki katika lugha. Pia walimu wanasema mpangilio wa mada pia unakanganya.

Maoni sawa na hayo yalitolewa na walimu kutoka pembe tofauti nchini ambao walisema tatizo hilo haliko kwa vitabu vya Kiswahili pekee mbali pia katika vile vya masomo ya Kiingereza, Hesabu, Fizikia, Kemia na Biolojia.

 

Kuchanganyika

Suala lingine ambalo walimu wamezua ni kuwa baadhi ya mada zimechanganyika ambapo zinazopasa kufunzwa katika vidato cha pili hadi nne vimo katika vitabu vya kidato cha kwanza.

“Matatizo mengine yaliyopo yanahusu ufinyu wa mada. Hakuna maelezo ya kina. Wachapishaji waliharakisha bila kupitia ile kazi waliyokuwa wakichapisha. Hii inaathiri wanafunzi kwa sababu wanasoma mambo ambayo hayawafai ama yanawapotosha,” akasema.

Afisa anayesimamia utafiti katika Taasisi ya Kenya ya Uundaji wa Mtaala (KICD), Bw Cyril Oyuga, alikiri kwamba taasisi hiyo imefahamu kuna dosari katika baadhi ya vitabu na tayari kuna mikakati iliyowekwa kusahihisha makosa.

Hata hivyo, alisema vitabu hivyo vilikuwa bora zaidi miongoni mwa vile vilivyotathminiwa wakati wa utoaji zabuni na makosa yaliyopatikana ni machache yasiyoweza kuathiri elimu ya wanafunzi.

WANAFUNZI wa Kidato cha Kwanza katika shule ya Moi Girls, Eldoret wakionyesha vitabu walivyopewa chini ya mpango wa Serikali mapema mwaka huu. Walimu wamelalamika kuwa baadhi ya vitabu hivyo vina makosa yanayopotosha wanafunzi. Picha/Jared Nyataya

Marekebisho

“Kuna makundi ambayo tayari yameundwa kufanya utathmini kuhusu makosa hayo na wanafanya marekebisho. Hilo litatatuliwa,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Kulingana naye, itaamuliwa baadaye kama vitabu husika vitahitaji kubadilishwa au walimu watafahamishwa kuhusu marekebisho yanayofaa kufanywa.

“Tunakiri kwa sasa kuna makosa machache. Kama kuna chochote cha ziada watakachoona walimu tunaomba wawasiliane nasi kisha tutazidi kuboresha vitabu hivyo,” akasema.

Mpango wa kusambaza vitabu milioni 33 shuleni ulinuiwa kufanikisha lengo la Serikali ya Jubilee ya kutoa elimu bora bila malipo kwa kila mtoto, hasa kwa watoto wanaotoka katika jamii zisizojiweza kimapato.