Habari Mseto

Vitabu vya gredi ya nne vya mfumo wa CBC kusambazwa

November 7th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

VITABU vya gredi ya nne – darasa la nne – katika mfumo unaotia zingatio katika uamilifu (CBC) vitasambazwa kwa muda wa miezi miwili ijayo.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, imefafanuliwa kwamba hii ni baada ya serikali kununua vitabu vya kusoma (textbooks) vya shule zaidi ya 22,000 nchini katika mchakato utakaokamilika mwishoni mwa mwezi Novemba.

Hii ni kufuatia maagizo ya serikali kwa Taasisi ya Kuandaa na kukuza Mtaala Nchini (KICD) na wachapishaji kuwa shughuli hiyo ifanyike bila kuchelewa.

Haya yalijadiliwa katika mkutano uliofanyika katika makao makuu ya KICD.

Naibu mkurugenzi wa masomo ya shule za msingi katika Wizara ya Elimu Bi Nereah Olick alisema kuwa orodha ya wanafunzi katika kila shule tayari imekabidhiwa wachapishaji.

“Orodha hiyo itasaidia katika kujua idadi ya wanafunzi ili kuhakikisha kuwa hakuna uchapishaji wa vitabu kupita idadi inayofaa,” alisema Bi Olick.

Bi Olick aliwahimiza wachapishaji kuwa tayari kuwasiliana kuhusu changamoto zitakazowakumba na kuwa wizara hiyo inaunga mkono shughuli hiyo.

Aliwaonya wachapishaji kuwa hakutakuwa na kuongezewa kwa muda zaidi ya uliopeanwa wa uchapishaji.

“Ni jukumu lenu kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa vitabu hivyo vinafika katika shule mbalimbali kwa muda unaofaa,” akasema mkurugenzi mkuu wa KICD Dkt Julius Jwan.