Habari

Vitambulisho hukosesha maelfu mikopo ya Helb

July 13th, 2019 1 min read

Na FAITH NYAMAI

MAELFU ya wanafunzi wa vyuo kikuu walio na umri wa chini ya miaka 18 hawapati mikopo ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (Helb) kila mwaka kwa kukosa vitambulisho vya kitaifa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Helb, Charles Ringera, alieleza Taifa Jumapili kwamba takriban wanafunzi 8,000 hukosa mikopo hiyo kila mwaka kwa sababu hawajahitimu umri wa miaka 18 ili kupata vitambulisho vya kitaifa.

Katika mwaka huu wa 2019 pekee, idadi ya wanafunzi ambao hawakufanikiwa kupata mikopo hiyo kwa kukosa vitambulisho ilikuwa 2,000.

Idadi hiyo inatokana na wanafunzi wanaokamilisha kidato cha nne kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

Wizara ya Elimu imekuwa ikitahadharisha kuhusu hatua ya wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni wakiwa na umri mdogo.

“Sheria inasema ili uingie katika mkataba ni lazima uwe umehitimu umri wa utu uzima unaoothibitishwa na nambari ya kitambulisho cha kitaifa. Ikiwa utafanya mkataba na mtoto kandarasi hiyo haitambuliwi kisheria,” alisema Bw Ringera.

Kujiandikisha

Vilevile, alisema kwamba ijapokuwa muda wa kujiandikisha kwa mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu huisha Julai 31, kwa kawaida bodi ya mikopo huwapa wanafunzi watakaopata vitambulisho vyao kati ya Julai na Desemba muda mfupi wa kujiandikisha kwa mikopo hiyo baada ya kupata stakabadhi hiyo.

Wanafunzi ambao hawapati vitambulisho vyao katika muda huo hulazimika kusubiri hadi mwaka unaofuata.

Bw Ringera alisema miongoni mwa wanafunzi 2,000 waliojisajilisha mwaka huu, wale ambao hawatakuwa wamepata vitambulisho vya kitaifa watazingatiwa katika bajeti ya 2020. Alisema kufikia sasa, Wizara ya Elimu imekuwa ikijitahidi kusuluhisha tatizo hilo.