HabariSiasa

Vitisho vya Jaguar vyaitia TZ tumbo joto

June 25th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa bunge la Tanzania Job Ndugai ameitaka serikali ya nchini humo kutoa taarifa kuhusu usalama wa Watanzania wanaoendesha biashara nchini Kenya baada ya Mbunge wa Starehe Charles Njagua kuapa kuwafurusha raia wa kigeni wanaoendesha biashara Nairobi.

“Naitaka serikali kutoa taarifa ya haraka kuhusu suala hili kwani ni wazi kuwa maisha ya watu wetu wanaoendesha biashara nchini Kenya huenda yakawa hatarini,” Bw Ndugai akanukuliwa na gazeti la The Citizen.

Suala hilo liliibuliwa na Mbunge wa Rufiji Mohemmed Mchengerwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mbunge huyo alitafuta ushauri kutoka kwa Spika baada ya kutazama video iliyosambazwa mitandaoni ikimwonyesha Bw Njagua akitoa vitisho dhidi ya wafanyabiashara wageni.

Spika Ndugai alisema japo hajatazama kanda hiyo, ameshawishika kuwa serikali ya Tanzania inafaa kutoa taarifa kwa haraka kuhusu vitisho hivyo.

Spika wa bunge la Tanzania Job Ndugai. Picha/ Hisani

Mnamo Jumatatu Mbunge huyo wa Starehe alizuru eneo la kibiashara la Kamukunji Trading Centre kufuatia malalamishi kutoka kwa wafanyabiashara kwamba wageni wamevamia eneo hilo na wanaendesha biashara ambazo zinapasa kuendeshwa na Wakenya.

Akiwahutubia wafanyabiashara hao, Bw Njagua, maarufu kama Jaguar, alitoa makataa ya saa 24 kwa serikali kuwafurusha wafanyabiashara wageni la sivyo awaondoe kwa nguvu.

“Juzi Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alitangaza kuwa amewafuruha wafanyabiashara sita wa China. Ningependa kumwambia kwamba wale tunaowalenga sio hao pekee, bali mamia ya wageni ambao wamekufurika nchini, hasa hapa Nairobi,” akafoka Bw Jaguar ambaye alionekana kuwa na hasira.

“Naipa serikali saa 24 kuwafurusha, la sivyo tutavamia biashara zao na kuwaondoa kwa nguvu, na kuwapeleka uwanja wa ndege. Kazi ya Matiang’i na Idara ya Uhamiaji itasalia ni kuwaweka kwenye ndege na kuwarejesha makwao,” mbunge huyo akaongeza.

Bw Njagua alikuwa ameandamana na Mbunge wa Langata Nixon Korir na Tindi Mwale wa Butere.

Alisema kuwa kuachiliwa kwa Kontena kutoka depo ya Embakasi kama alivyoagiza Rais Uhuru Kenyatta haitakuwa na maana yoyote ikiwa wafanyabiashara kutoka mataifa ya kigeni wataendelea kushindana na wenyeji.