Makala

Vitu kwa ‘ground’: Mlimani sasa waanza kumfasiri Ruto kama ‘adui’ wao kisiasa

Na MWANGI MUIRURI August 21st, 2024 2 min read

RAIS William Ruto sasa anaonekana kuwa adui wa kisiasa wa wakazi wa Mlima Kenya kutokana na ukuruba wake na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Katika chaguzi nne zilizopita Bw Odinga amekuwa akinadiwa kama ‘adui’ wa eneo hilo na wanasiasa wengi wamejijengea sifa kwa kumpiga vita kisiasa.

Hatua ya Rais Ruto kuridhiana kisiasa na Bw Odinga imewashangaza viongozi wa Mlima Kenya akiwemo Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiasi cha wadadisi kubashiri kuwa huenda eneo hilo likamuunga mkono mpinzani wa Dkt Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), Bw Charles Mwangi , anasema itakuwa vigumu kwa Rais Ruto kugeuza dhana ya wakazi wa Mlima Kenya kuwa amewasaliti na sasa ni ‘adui’ wao alivyokuwa Bw Odinga katika chaguzi zilizopita.

“Ukisikiza sauti za raia maeneo ya mashinani katika Mlima Kenya, wengi wamehamisha hasira na chuki zao kutoka kwa Bw Odinga hadi kwa Rais Ruto. Hii ni kutokana na masuala ya uongozi yaliyochochea maandamano ya Gen Z yaliyoshudiwa hata katika miji kadhaa ya Mlima Kenya ambako fujo kama hizo hazijawahi kuonekana miaka ya nyuma,” Bw Mwangi anasema.

Anaongeza kuwa kuundwa kwa baraza jipya la mawaziri, lililoshirikisha wandani wa Bw Odinga, kulionekana kama dharau kwa eneo hilo lililompa Rais asilimia 42 za kura katika uchaguzi uliopita wa urais.

Kwa upande wake, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Bw Gasper Odhiambo, ameiambia Taifa Leo kuwa huenda wakazi wa eneo la Mlima Kenya wakasusia uchaguzi mkuu kama njia ya kumwadhibu Rais Ruto.

“Wengine huenda wakampigia kura Bw Odinga akiwania tena endapo atakosa kiti cha mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC). Sababu ni kwamba baada ya wao kumwangusha, hurejea mezani na kumegewa minofu serikalini,” anaeleza.

“Ikiwa kuna hasira ambazo zitawafanya wakazi wa Mlima Kenya kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa urais 2027, basi zitakuwa ni za kumwangusha Rais Ruto kulipiza kisasi usaliti wa 2022,” Bw Odhiambo anaongeza.

Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee, Bw Jeremiah Kioni, anasisitiza kuwa mnamo 2027, “wakazi wa Mlima Kenya wataungana dhidi ya uongo wa kisiasa na uongozi mbaya unaoendelezwa na serikali hii”.

Mbunge huyo wa zamani wa eneo la Ndaragua, anabashiri kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba mwaniaji mkuu wa urais atakayempinga Rais Ruto na serikali yake mnamo 2027, atashinda.

“Upigaji kura hautaongozwa tena na chuki dhidi ya Bw Odinga bali chuki na hasira dhidi ya Dkt Ruto na utawala wake,” Bw Kioni anaeleza.

Kulingana naye, wakazi wa Mlima Kenya sasa wameeruvuka; hawatakubali tena kudanganywa kwani wameamua kwa kauli moja kupinga serikali hii.

Lakini msimamo huu unapingwa na Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Bw Hassan Omar, akisema hauna mashiko.

“Hamna kiongozi atakayekuwa na uwezo wa kutumia kadi ya ukabila kushawishi mkondo wa siasa katika eneo lolote nchini,” Bw Omar akaambia Taifa Leo.

“Siasa ni telezi. Wale ambao wanadhani wanaweza kutumia kelele kupata uungwaji mkono na kupanda mbegu za migawanyiko watagundua kuwa mbinu kama hizo hazitadumu,” akaongeza.