Makala

VITUKO: Msodai apeleka wanafunzi Pwani badala ya shambani kwa Delameya

September 18th, 2019 2 min read

Na SAMUEL SHIUNDU

‘SIKU ya kufa kwa nyani, miti yote huteleza’ ni msemo ambao Msodai alizoea kuusikia bila kuutilia maanani.

Aliuona kama msemo tu uliowahusu nyani na miti porini.

Kamwe hakuwahi kufikiria kuwa ukweli wa msemo huo kwa binadamu ungemdhihirikia kwa namna ulivyomdhihirikia ziara yake ya zaraa ilipotibuka.

Alipokuwa akizifuja pesa alizoletewa na wanafunzi na zilizonuiwa kufadhili ziara yenyewe, hakuwa na wasiwasi kabisa.

Alijua kuwa alilokuwa akilifanya lilikuwa kosa dogo likilinganishwa na makosa ya mkuu wake kazini pamoja na mwalimu Sindwele. Alijua kuwa wawili hawa pekee ndio walioweza kumuuliza kuhusiana na fedha hizo naye alikuwa na dawa mujarabu kwao.

Alijua kuwa angewanyamazisha walimu hao kwa kuwazulia kashfa.

Wakati huo, aliamini kuwa starehe za likizo ya Aprili kati ya Simba na Asumini kule Pwani zilikuwa zinafadhiliwa na pesa za shule. Alihitaji tu kumnunulia mhasibu wa shule bia mbili ili kumwezesha kuropoka. Kwa upande wa Sindwele, alikuwa kupanga kumbomoa kwa kutumia karatasi za wanafunzi zilizokuwa zimesahihishwa kiholela na huyo rafiki mkubwa wa bwana hedimasta.

Hivyo ndivyo Msodai alivyopanga kuififisha kashfa yake kwa kuwazulia wenzake kashfa. Lakini baada ya kuufanya uchunguzi wake kuhusiana na likizo ya Simba, alikuja kugundua kuwa likizo hiyo ilikuwa imegharimiwa na binti Asumini.

Simba hakutumia hata senti moja ya shule. Isitoshe, karatasi za wanafunzi alizotaka kuzitumia kama ushahidi dhidi ya Sindwele nazo zilikuwa zimetoweka. Walimu na wanafunzi hawakuwa tayari kughushi karatasi nyingine kwani Msodai alikwishaiharibu imani yao kwake tangu afuje pesa za ziara.

Masaibu ya Msodai hayakuishia hapo, wanafunzi hawakutaka kusikia habari za kufidiwa pesa. Walichokitaka ni ziara. Msodai hakuwa na budi kutafuta pesa za kugharimia ziara nyingine.

Hili nalo likamkosesha usingizi kwa siku kadhaa, usicheze na elfu thelathini katika kipindi hiki cha tarehe kumi na…

Alilazimika kuchukua mikopo ya simu kupitia huduma za MShwari, Tala na KCB M-Pesa.

Hatimaye akaambulia elfu ishirini. Aliwaza na kuwazua na hatimaye akaamua kutumia mbinu zote alizozijua kuyabana matumizi.

Kwa vile hakuwa na pesa ya kutosha kuwalipia ada ya kiingilio katika shamba la Bwana Dalameya kama alivyokadiria awali, akaamua kuwapeleka Pwani. Huko asingehitaji ada ya kiingilio.

Japo Pwani hakukufaa kwa ziara ya zaraa, aliona kuwa nusu shari ni heri kuliko shari kamili. “Huenda nami Mungu akanikutanisha na Asumini wangu huko” alijiambia.