Makala

VITUKO: Pengo atua Migingo, kumbe tabasamu ya kike hunogesha biashara ya samaki!

September 9th, 2020 2 min read

Na SAMUEL SHIUNDU

KAMA ardhi ya kisiwa cha Migingo ingekuwa na hisia, basi ingelalamikia kupondwa na nyayo nyingi kiasi hicho.

Tangu majilio ya corona, Pengo alikuwa hajawahi kuona hadhara ya watu wengi kiasi kama kile kilichokuwa hapo kisiwani Jumatano hiyo.

Walikuwepo wavuvi wakinadi samaki wao, walikuwepo mama ntilie waliouza vyakula kwa wanabiashara wa samaki, walikuwepo wanunuzi wa samaki waliokuwa wakibisha ili wauziwe bidhaa hiyo kwa bei nzuri ili nao waambulie faida watakapouza baadaye. Kila mtu na hamsini zake.

Wengi wa wanabiashara wa samaki walikuwa watu waliokula wakashiba. Wavuvi walikuwa wanaume wenye misuli iliyotutumuka kama ya waambua vyuma, wateja nao walikuwa wanawake waliofungasha si mchezo. Wote walikuwa na nyuso zinazomwekamweka. ‘Wanakula nini hawa wanabiashara wa samaki?’ Pengo alijiuliza huku akiangaza macho huku na kule kumtafuta mvuvi ambaye angemfaa kwa kumuuzia samaki wazuri.

Pengo aligundua kuwa wavuvi hao walikuwa na mapendeleo fulani. Waliwaona wateja wa kike tu. Wakawaita na kuwahudumia kwa haraka. Akiwa mtu ambaye hakuzoea kuwabembeleza binadamu wenzake, hasa wanaume, Pengo aliendelea kuzunguka pale kisiwani kama mwana mpotevu. Haukuchukua muda, akawa kachoka tiki! Akaingia kwenye kibanda kimojawapo ili ajitafutie chochote cha kulinyamazisha tumbo lake ambalo lilikuwa limeanza kuilalamikia njaa.

Alipotiliwa chakula, akamuuliza mwenyeji wake sababu ya kupuuzwa na wavuvi, “Akina mama wote tuliofika nao na wale walionipata hapa wameshajiondokea na mizigo yao, mimi hakuna mvuvi aliyenitupia jicho na kuniuliza nitakacho. Hivi nina alama ya shari au vipi?”

Mwenyeji wake aliangua kicheko na kumuuliza, “Kumbe wewe mgeni hapa kisiwani? Macho ya wavuvi hayajaumbiwa watu kama wewe. Ungekuwa mwanamke ungekuwa njiani ukirejea kwenu na zigo lako la samaki,”

“Sijakuelewa mama” Pengo alimjuza.

“Hapa kisiwani, mwanamke na tabasamu yake ni mfalme.” Mama ntilie alimfichulia hatimaye.

Pengo hakuwa mgeni katika dunia hii inayoamini kuwa mwanamke mzuri ni silaha, lakini pia aliwafahamu wanaume walioiendesha biashara hii ya samaki huko kwao. “Hawa waliwapata wapi samaki?” akauliza.

“Hiyo ndiyo kazi yetu nyingine, kuwanunulieni watu kama nyinyi samaki. Leta elfu tano nikakuletee gunia la samaki sasa hivi.”

Pengo alitaka kubisha jinsi alivyowaona wanawake wakibishana na wavuvi kule nje. Alitaka apunguziwe bei. Akafungua kinywa lakini akashtuliwa na mmoja wa wateja wa hapo, “Habari ya mwalimu?” Aliamkiwa na mteja huyo. Akaufyata. Alijiambia kuwa mwalimu kama yeye hakupaswa kulialia.