Makala

VITUKO: Sindwele akutikana barabarani si wa maji si wa chakula, adhaniwa kafariki

February 20th, 2019 2 min read

Na SAMUEL SHIUNDU

TANGU atuhumu njama ya kufurushwa shuleni, Sindwele alijikakamua kutekeleza wajibu wake wa ualimu kama alivyotarajiwa.

Alifika shuleni kila siku bila kuchelewa, aliandika maazimio ya kazi, akaandika mpangilio wa somo na kuandika rekodi za kazi zilizotelekezwa jinsi ilivyohitajika kwa mwalimu yeyote.

Alichora mabango na kubeba nyenzo zilizohitajika ili kuboresha vipindi.

Yote tisa, kumi ni kwamba alisusia kuingia baani na kwenye maeneo mengine ya burudani. Tabasamu Lililokuwa limetoweka usoni mwa Sofia lilirejea.

Hakumchukia mumewe tena. Alimpenda kwa dhati jinsi alivyompenda katika siku za uchumba wao. Sindwele alijiweka katika hali hii nzuri hadi awamu ya kwanza ya muhula wa kwanza ikaisha vyema.

Mkewe alienda kanisani akapiga magoti na kumshukuru Mungu. Aliuona ulevi wa awali wa mumewe kama upele ambao ulikuwa umepata mkunaji.

Hata hivyo, furaha ya Sofia ilikuwa ya muda tu. Likizo fupi ilipong’oa nanga, mumewe alirejelea sehemu zake za burudani.

Siku moja alialikwa Jamhuri na rafiki yake ambaye alikuwa kapata hela baada ya kuuza miwa.

Kwa kuwa hela alizopewa zilikuwa kidogo kuliko alivyotarajia, aliamua kuwa hangefika na vipeni hivyo vichache nyumbani, akamwaalika Sindwele kwenye baa ya Jamhuri.

“Mletee huyu bwana sharubati. Nasikia siku hizi kapishana na ulevi,” mdhamini wa Sindwele alitoa maagizo kwa mhudumu.

“Wewe usimsikilize huyu bwana. Niletee kinywaji cha kiume. Nikiacha pombe nitakufa aisee!” Sindwele akamjuza mhudumu.

Chupa kadhaa za mvinyo zikamsahaulisha Sindwele kwamba alipaswa kurejea nyumbani. Akaendelea kubugia hadi akajisahau kabisa. Hakujua kilichomfanyikia hadi alipojuzwa siku mbili baadaye.

Mwili wa mwanamume mzima ambaye hakutambulikana ulikutika katikati ya barabara kuu kijijini Maka. Dalili zote zilionyesha kwamba mwanamume huyu kafa.

Hakuna aliyemkaribia mwanamume huyu kwani watu wa Maka waliogopa kisirani cha kumgusa mfu.

Wakaitwa polisi. Polisi walipofika, wakamzungushia utepe na kusubiri kando ya huo mwili wenyewe kwani na wao hawakuwa na uhakika kama huyo mtu kakata roho au la.

Aliyedhaniwa kukata roho alianza kulalamikia baridi.

Alijipugapunga kujiondolea mbu na kulalamika kuwa mkewe alikuwa kamhini kwa kumnyang’anya blanketi. Akapapasapapasa huku na kule kulitafuta hilo blanketi asilipate.

Mkono wake ukakutana na kitu alichokiamini kuwa ni blanketi akakivuta kwa fujo.

Polisi aliyeketi akisinzia kando yake alizinduliwa na fujo hizo za mlevi aliyekuwa akivuta kabuti lake kwa fujo. Polisi wakajua kuwa mtu wao hakuwa amekata roho bali alikuwa kalewa tu na sasa alikuwa ameleuka. Wakamtia pingu na kumpeleka selini.