VITUKO: Sogora King Kazu atachoka na mpira siku akifikisha umri wa miaka 60

VITUKO: Sogora King Kazu atachoka na mpira siku akifikisha umri wa miaka 60

IMEKUSANYWA NA CHRIS ADUNGO

FOWADI Kazu Miura, 55, ndiye mwanasoka mkongwe kabisa duniani anayezidi kutamba uwanjani!

Amini usiamini, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 55 ametia saini mkataba mpya utakaofanya usogora wake kuwa miaka 37!

Miura, aliyechezea timu ya taifa ya Japan kwa zaidi ya miaka 10, alianza kusakata kabumbu kitaaluma akivalia jezi ya klabu ya Santos nchini Brazil mnamo 1986.

Tangu wakati huo, amebadilisha klabu mara 14 japo alichezea Yokohama FC kwa miaka 17 kabla kutumwa Suzuka Point Getters FC kwa mkopo mwaka 2023.

Kazu, atakayefikisha umri wa miaka 56 mwezi huu, amefichua mpango wa kustaafu soka pindi atakapotimu umri wa miaka 60.

Alipata fursa ya kuchezea klabu ya 15 tofauti wiki hii baada ya kusajiliwa na Oliveirense ya Ureno kwa mkopo.

Mechi yake ya kwanza kambini mwa Oliveirense itakuwa leo dhidi ya Vilafranquense inayoshiriki pia Ligi ya Daraja ya Pili.

Miura, almaarufu King Kazu, alikuwa tayari anatandaza boli kabla ya Lionel Messi kuzaliwa. Ndiye mwanasoka mkongwe zaidi katika historia kuwahi kufunga bao katika Ligi Kuu ya Japan (J-League). Alichezea timu ya taifa ya Japan kati ya 1990 na 2000 akifunga mabao 55 kutokana na mechi 89.

Kigogo huyo aliwahi kufungia Verdy Kawasaki FC mabao 117 kutokana na mechi 192 na kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka kutoka bara Asia mnamo 1992. Ufanisi huo ulimfungulia mlango wa kuchezea Genoa ya Italia kabla ya kujiunga na Dinamo Zagreb ya Croatia.

Alirejea Japan mnamo 1999 kuvalia jezi za Kyoto Sanga kabla ya kuingia katika sajili rasmi ya Vissel Kobe kisha Yokohama mnamo 2005.

Alichezea timu ya taifa ya Japan kati ya 1990 na 2000 na akapachika wavuni mabao 55 kutokana na mechi 89.

Hata hivyo, hakuwahi kunogesha fainali za Kombe la Dunia baada ya Japan kutofuzu kwa kipute hicho mnamo 1994 huku akiachwa nje ya kikosi kilichotegemewa na taifa hilo nchini Ufaransa mnamo 1998.

  • Tags

You can share this post!

Benki ya CIB yasifu Kenya kwa ustawi wa upesi kidijitali

STAA WA SPOTI: Huyu fowadi Felix Ojow ni moto otea mbali...

T L