Makala

VITUKO: Tangazo la gavana wa benki kuu lahangaisha mgema wa Sindwele

June 5th, 2019 2 min read

Na SAMUEL SHIUNDU

TANGU sherehe za kuadhimisha miaka hamsini ya uhuru wa taifa lao, suala la kubadilishwa kwa sura ya pesa liliyatawala mazungumzo ya watu.

Popote walipokusanyika watu wawili au watatu, mada ya sura mpya ya pesa ilikuwa kati yao.

Suala hili liligeuzwa ndani nje na nje ndani kisha likachanganuliwa kwa mapana na marefu.

Kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, Simba na Sindwele walikuwa wameihama baa ya Rijino.

Walikuwa wamepagundua mahali pengine nafuu.

Kando na bei yake nafuu, Asumini alikuwa mwingi wa bashasha.

Alikuwa ndipo katua kijijini Bushiangala kutoka pwani. Alichokuwa akikifanya pwani alijua yeye na Mungu wake.

Licha ya uneni wake mwingi, hakuligusia suala hili na kwa bahati nzuri, hakuna yeyote katika wateja wake aliyejishengesha nalo.

Wengi lakini walivutiwa na uzuri wake.

Uzuri ambao ulikuwa ka kipekee, uzuri ambao hata kipofu angeuona.

Simba alikuwa miongoni mwa watu waliovutiwa.

Hakukijua hicho kilichomneemesha mwenzake lakini alikuwa na uhakika kuwa chochote alichofanya hakikuwa halali na ndiposa alikuwa msiri kiasi hicho.

Kwa upande wake, kitendo cha mhudumu wa Rijino kumwekea simu kilikuwa kimetishia kusambaratisha uhusiano kati ya Sindwele na mkewe.

Alilazimika kutumia kila tendo la unyenyekevu alilolijua kuomba msamaha, hatimaye akaapa kuwa hangeutia mguu wake Rijino tena.

Barazani kwa Asumini, Simba na Sindwele walilijadili suala la kubadilisha pesa na kulihusisha na vita dhidi ya pesa chafu zilizofichwa kwenye nyumba za wahuni.

Mazungumzo haya yalimsumbua mwenyeji wao.

Alikumbuka kisa cha, Pesa Zako Zinanuka alichowahi kukisoma.

Hakukikumbuka kisa chenyewe vyema lakini alikumbuka kiini chake.

Alimkumbuka mhuni aliyefuja pesa zilizotengewa dawa za watoto.

Hatimaye mwanawe fisadi huyo akafa kwa yayo hayo maradhi yaliyohitaji zizo hizo dawa. Alipojaribu kumshawishi mamake mtoto kwa pesa, mama mtoto alimkataa kwa kauli kwamba, ‘pesa zako zinanuka.’

Asumini aliziona pesa zake kuwa chafu. Alijua kuwa japo cha mlevi huliwa na mgema, yeye alikuwa kawahini wateja wake kupita kiasi.

Alikuwa na uhakika kwamba zipo pesa alizochukua kwa wateja wake zilizokusudiwa kulipa karo za watoto au kununua dawa kwa wagonjwa au chakula kwa wenye njaa.

Ni mara ngapi alikuwa kawapumbaza wateja wake na kuifagia mifuko yao? Sasa alikuwa kajaza maelfu katika mto wa kitanda chake.

Alilaghai na kulimbikiza maelfu bila kujiuliza kule ambako pesa zenyewe zingempeleka. Alimtaka Simba kwa mashauriano ya chemba.