Makala

VITUKO: Uadilifu wa Pengo wamvunia marafiki na mahasidi, maadui wapanga kumdamirisha

May 22nd, 2019 2 min read

Na SAMUEL SHIUNDU

TANGU arejee Sidindi kutoka Bushiangala, hajamjulia hali mwenzake wa dhati.

Kimya hiki kilitokana na kazi nyingi za shuleni Sidindi. Mwalimu mkuu wa Sidindi alikuwa na matumaini makuu kwa wanafunzi wake.

Matumaini haya yalimfanya awasukume walimu kufanya kazi kwa bidii. Kwake mwanafunzi alikuwa mfalme na mwalimu alijuzu kumtumikia.

Chochote ambacho wanafunzi walihitaji kilitekelezwa haraka iwezekanavyo hususan muhula huu wa pili wenye tishio la visa vya utovu wa nidhamu katika shule za upili.

Aliwateua baadhi ya wanafunzi kuipeleleza mienendo ya wanafunzi wenzao na hata walimu. Wapelelezi hawa walikuwa na satua hata kuliko walimu sikwambii viranja.

Kwa kuwa Pengo alikuwa na bidii za mchwa, mwalimu mkuu alimchukulia kama mwenza ambaye angemsaidia.

Pengo hakuwa kama walimu wengine hapo Sidindi. Alikuwa mwanamume aliyejihifadhi, si kama wanaume wenye macho yafwatayo kila uso wa msichana mzuri waliyepishana naye.

Mwalimu mkuu alimpenda Pengo kutokana na uadilifu wake, insafu yake na uchapakazi wake.

Yeye hakusukumwa kama wenzake, alijituma.

Hakuwekewa makataa, alijiwekea. Alipendwa na wengi wa wanafunzi.

Hata makachero wa mwalimu mkuu hawakumpelekea ripoti yoyote mbaya kumhusu huyu mwalimu. Huyu ndiye aliyekuwa Pengo, kipenzi cha wengi hapo Sidindi.

Uadilifu wavuna vyeo

Uadilifu wake ukamvunia vyeo tele.

Akateuliwa kusimamia michezo na shughuli za bweni hapo Sidindi. Waliokuwa wakizishikilia nyadhifa hizi awali hawakufurahi. Wakamtafutia njama.

Walitafutana na kushauriana kuhusu walichopaswa kufanya.

Wakakumbuka kwamba alipokuwa akiwaandaa wanafunzi kwa tamasha za drama na, alipiga marufuku suala la matumizi ya dawa za kulevya.

Lazima kuna wanafunzi walioumizwa na hili? Kama wapo basi lazima nao wana kisasi na hiki kimalaika cha mwalimu mkuu” walikubaliana.

Hawakutafuta sana. Alipatikana mwanafunzi aliyekuwa akiuza dawa hizi. Wakapatana naye. Akakubali.

Kwa vile aliaminiwa sana na wanafunzi, Pengo alikuwa akiwahifadhia wanafunzi pesa walizotumiwa na wazazi kwa ajili ya masurufu.

Pia, alitumwa kuwanunulia vitu walivyohitaji sokoni na kwenye maduka ya kijumla. Si kalamu, si vitafunwa na vipochopocho vingine. Na hapo ndipo walipokubaliana kumnasia huyu bwana Pengo.

Pengo hakushuku lolote Sande alipombishia akiomba kununuliwa sabuni mjini.

Sande alijulikana kwa kutofua wala kukoga. Alisisitiza asinunuliwe kwingine ila kwa duka la baniani maarufu hapo mjini.

“Tafadhali ninunulie kwa Mirza, bei yake ni nafuu.” Sande alirudia maneno aliyokuwa kapewa jana yake na walimu wawili waliomtwika jukumu hili na kumwahidi malipo. Pengo akaridhia.