Kimataifa

VITUKO UGHAIBUNI: Mwanamume afariki lojing'i akilamba uroda

May 21st, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

LIRA, UGANDA

POLISI wanachunguza kifo cha mwanamume mwenye umri wa miaka 38 aliyefariki katika chumba cha kukodisha mjini Lira baada ya kula uroda na mwanamke ambaye hajatambuliwa.

Msemaji wa polisi wa Kyoga Kaskazini, David Ongom Mudong, aliambia wanahabari Jumapili jioni kwamba mwili wa Ogwang Kizito, ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Alebtong, ulipatikana katika chumba kilicho Blue Valley Lodge katika barabara ya Olwol, mjini Lira.

“Maafisa wa polisi walienda katika eneo la mkasa wakapata simu ya rununu ya marehemu, kitambulisho cha kitaifa kilicho na majina ya marehemu, tembe za dawa na mipira ya kondomu iliyotumika,” akasema Bw Mudong.

Kulingana naye, haijafahamika wazi kilichosababisha kifo cha Ogwang kwani upasuaji wa kubainisha chanzo cha kifo chake unasubiriwa kufanywa.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Lira.

Msemaji huyo wa polisi aliongeza kuwa jamaa za marehemu walifahamishwa kuhusu kifo chake lakini hakuna mtu alikamatwa. Wasimamizi wa lojing’I hiyo waliandikisha taarifa kuhusu kifo hicho, kwa mujibu wa polisi.