Kimataifa

VITUKO UGHAIBUNI: Mwanamume huyu hulipa Sh292,000 kunyolewa

May 21st, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA na VALENTINE OBARA

NEW YORK, AMERIKA

BWANYENYE aliye raia wa Canada amefichua hutumia dola 2,920 (Sh292,000) kila mwaka kunyoa nywele.

Kevin O’Leary, 63, ambaye ni mashuhuri kwa ukwasi wake unaokadiriwa kuwa wenye thamani ya dola milioni 400 (Sh40 bilioni) na kushiriki kama mmoja wa majaji kwenye kipindi cha ‘Shark Tank’, alisema yeye huchukulia kwa umuhimu mkubwa nywele za kuvutia, hata ingawa ni kihara.

Kwenye mahojiano na shirika la habari la CNBC lililo Amerika, bwanyenye huyo alifichua huwa ananyolewa baada ya kila siku kumi, na hutumia dola 80 (Sh8,000) kila anaponyolewa.

“Mimi huwekeza katika hitaji la kuwa mtu wa kuvutia kila mara na huwa nafanya hivi kwa kuvaa nguo za kuvutia, viatu vizuri sana na kunyoa nywela kila baada ya siku kumi,” akasema.

Hata hivyo, aliongeza kuwa hapendi kunyoa kipara ambayo ni mtindo unaopendwa sana na wanaume wenye vihara.

“Sina nywele nyingi kwa hivyo huwa nataka kuwa na uhusiano na kila unywele kichwani mwangu. Watu huniuliza mbona nisinyoe nywele zote niwe kipara. Sipendi mtindo huo. Ninapenda mtindo huu. Nadhani navutia mno,” akasema.