Kimataifa

VITUKO UGHAIBUNI: Wanafunzi wanaotuonyesha mapaja wanatutesa – Mhadhiri

May 21st, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

KAMPALA, UGANDA

MHADHIRI wa kiume katika Chuo Kikuu cha Makerere amelaumu wanafunzi wa kike kwa kuwatia wahadhiri majaribuni wanavyovaa mavazi yanayowatia mahanjam.

Kulingana na ripoti ya kamati iliyokuwa ikichunguza visa vya dhuluma za kimapenzi chuoni humo, mhadhiri aliyehojiwa alisema hiafai wanawake kutembea wakionyesha mapaja yao wazi kila wanakoenda.

“Hawa ni maibilisi, washawishi wadogo wadogo wa kishetani ambao hukera wahadhiri wasio na hatia, wasio na uwezo wa kujilinda,” mhadhiri huyo ambaye hakutajwa jina alinukuliwa kusema.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Prod Sylvia Tamale ilipendekeza wafanyakazi chuoni wawe wakisema wazi wanapovutiwa kimapenzi na wanafunzi au wafanyakazi wenzao.

Ripoti hiyo ya mapema iliyotolewa Ijumaa ilibainisha kuwa dhuluma za kimapenzi chuoni zimeenea kuliko inavyofahamika rasmi.

Asilimia 80 ya watu 234 waliohojiwa na kamati hiyo walisema wanafahamu kuna dhuluma za kimapenzi ikiwemo kutoka kwa wahadhiri wanaoitisha ngono kutoka kwa wanafunzi ili kuwaongeza alama.

Katika visa vingine, waliohojiwa walisema wanafunzi wa kike hudhulumiwa na wahadhiri wa kiume ambao hudai mavazi yao si nadhifu.

Baadhi ya waliohojiwa walipendekeza chuo kiwe na mwongozo kuhusu mavazi yanayofaa kuvaliwa chuoni.

Prof Tamale ambaye ni msomi wa kisheria alisema hakuna ushahidi wowote wa kisayansi kuthibitisha kuwa mtindo wa mavazi huwa ni chanzo cha dhuluma za kimapenzi, akaongeza kuwa hakutakuwa na mwongozo wowote wa mavazi chuoni kwani kuna sababu nyingine ya dhuluma za kimapenzi.