Habari Mseto

Vituko vya mastaa: Mke sasa afichua Pogba amesusia miereka ya mle chumbani

April 6th, 2024 1 min read

NA CHRIS ADUNGO

KIDOSHO Maria Zulay Salaues amemtaka mumewe Paul Pogba kujituma kiume katika masuala ya chumbani licha ya wingu jeusi linalozingira taaluma yake.

Kiungo huyo mahiri wa Ufaransa alipigwa marufuku ya kucheza soka kwa miaka minne mwezi uliopita baada ya kupatikana na hatia ya kutumia dawa haramu za kusisimua misuli za DHEA.

Katika mahojiano na gazeti la The Sun wiki hii, Maria alifichua kuwa mumewe amebadilika sana tangu apokezwe adhabu hiyo kiasi kwamba amesusia mahaba aliyohusudu sana awali na “hakuna chochote kinachomsisimua kwa sasa.”

“Nazidi kumhimiza awe na moyo wa ujasiri. Naendelea kumtia nguvu kadri ya uwezo wangu. Nimetafuta pia marafiki kadhaa wa karibu ambao humzungumzia mara kwa mara,” akasema Maria.

Mwezi mmoja uliopita, Maria alishauri Pogba, 31, afikirie kuangika daluga zake ili naye “apate fursa ya kuona raha chumbani kama wanawake wengine”.

Iwapo ataruhusiwa kurejea uwanjani baada ya marufuku, Pogba, atakuwa na miaka 34. Ukweli huo, kwa mujibu wa The Sun, ndio ulimchochea Maria kumtaka mumewe astaafu ili wapate muda zaidi kujaza dunia wakiwa na “nguvu za ujana”.

Juventus, ambao ni waajiri wa sasa wa Pogba, bado hawajatoa tamko lolote kuhusu masaibu ya kiungo huyo wa zamani wa Manchester United.

Hata hivyo, magazeti mengi ya udaku nchini Italia na Ufaransa yanadai kuwa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kinajiandaa kusitisha mkataba wa Pogba “hivi karibuni”.

Miaka miwili iliyopita, Maria, ambaye ni raia wa Bolivia, alimpa Pogba masharti makali kabla ya kumzalia kimalaika kingine. Alimtaka pia sogora huyo kuchanja chale za kudumu zenye mchoro wa jina ‘Maria’ kifuani ili kudhihirisha ukomavu wa penzi lao.

Pogba alifunga pingu za maisha na kisura huyo mnamo 2019 baada ya kuchumbiana kwa muda mrefu. Wamejaliwa watoto wawili – Labile Shakur na Keyaan Zaahid.