Habari Mseto

Vituo mbalimbali Busia vyakabiliwa na upungufu wa damu katika hifadhi zao

July 17th, 2020 2 min read

SHABAN MAKOKHA na SAMMY WAWERU

VITUO vya afya katika Kaunti ya Busia vinakabiliwa na hali ya upungufu wa damu katika hifadhi baada ya shule na taasisi za elimu kufungwa kufuatia mkurupuko wa Covid-19 nchini tangu Machi 2020.

Afisa msimamizi wa kituo cha utoaji damu eneo hilo, Rosemary Okuku, amesema janga la corona limesababisha wenyeji kuwa na hofu, na kukataa kuzuru vituo vya afya kujitolea kusambaza damu.

Alisema kituo hicho kinategemea msaada wa watu wachache wanaojitolea na jamaa za wagonjwa wanaohitaji damu.

“Tulikuwa tukipata msaada wa damu kutoka kwa wanafunzi wa shule za upili, taasisi za elimu ya juu na pia wafungwa katika jela. Tangu ugonjwa wa Covi-19 uripotiwe nchini, watu wanaogopa kutembelea vituo vya afya kwa hofu ya kuambukizwa virusi vya corona,” Okuku akasema.

Kwenye mahojiano, afisa huyo alisema Hospitali ya Rufaa ya Busia inahitaji painti 20 za damu kila siku, na kwamba tangu janga la corona liripotiwe kutua nchini imekuwa vigumu kupata painti moja.

Okuku alieleza wasiwasi kwamba wagonjwa hasa manusura wa ajali, kina mama wajawazito na wanaougua ugonjwa wa ukosefu wa damu ya kutosha mwilini, ndio Selimundu, huenda wakapoteza maisha yao kufuatia upungufu wa damu unaoendelea kushuhudiwa.

Afisa huyo amewaomba wakazi na pia wasamaria wema kujitolea kuzuru vituo vya afya kusambaza damu, ili kuokoa maisha ya wanaohitaji damu. Amewahakikishia usalama wao katika vituo vya afya.

“Wengi wanahofia wakitembelea vituo vya afya watapimwa corona. Hata hivyo, kama wataalamu wa afya hatuwezi kulazimisha watu kupimwa. Isitoshe, tumeweka mikakati kabambe kuhakikisha wanaofika vituoni ni salama,” Okuku akaongeza.

Busia ni kati ya kaunti zilizoorodheshwa kuwa na idadi ya juu ya visa vya maambukizi ya Covid-19, ambapo ni ya tatu baada ya Nairobi na Mombasa, wengi wa waathiriwa wakiwa madereva wa matrela.

“Kwa sasa hali Buia ni mbaya kabisa, hazina ya damu tuliyokuwa nayo imeisha,” Okuku akasema.

Kauli ya afisa huyo imejiri wiki kadhaa baada ya Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya Dkt Rashid Aman kukiri Kenya ina upungufu wa damu, tangu corona iingie nchini.