Makala

Vituo vipya vya treni Ruiru na Githurai kusaidia kupunguza msongamano Thika Road

October 15th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

BAINA ya Jumatatu na Ijumaa Thika Superhighway hushuhudia msongamano mkubwa wa magari kwa kile kinatajwa kama ongezeko la magari yanayohudumu katika barabara hiyo kuu.

Thika Superhighway inaunganisha mitaa mbalimbali kama vile Githurai, Ruiru, Juja na Thika na jiji kuu la Nairobi.

Wengi wa wakazi wa maeneo hayo wanafanya kazi jijini, na majira ya asubuhi misafara mirefu ndiyo kibwagizo.

Licha ya ushirikiano wa serikali ya Kaunti ya Nairobi na ile ya kitaifa kujaribu kutafuta suluhu, juhudi hizo hazijazaa matunda yoyote.

Aidha, kati ya Roasters na Drive In, kuna miradi ya ujenzi wa vivukio viwili na mzunguko inayoendelea lengo likiwa kuona iwapo msongamano unaoshuhudiwa utapungua.

Ili kupiga jeki shabaha hiyo, serikali ya kitaifa imejenga vituo viwili vya garimoshi katika mtaa wa Githurai na Ruiru, yote ikiwa kaunti ya Kiambu.

Shughuli hiyo iliyong’oa nanga 2017 iko katika muda wa lala salama, miradi kukamilika.

Hata ingawa kiasi cha fedha zilizotumika kuufanikisha hakijabainika, mbunge wa Ruiru, Simon King’ara anasema vituo hivyo vitazinduliwa hivi karibuni, baada ya vifaa vyote kuwasilishwa.

“Serikali iko katika harakati za kununua magarimoshi 11 ya abiria yatakayohudumu kati ya Ruiru, Githurai na Nairobi,” akasema.

Akipigia upatu vituo hivyo vya reli, Bw King’ara anasema vitasaidia kupunguza misongamano katika barabara kuu ya Thika Superhighway.

Mapema Oktoba 2019 mbunge huyo pamoja na Katibu katika Wizara ya Ujenzi anayehusika na miundomsingi, Bw Charles Hinga, walifanya ziara katika vituo hivyo kukagua hali yake.

Maeneo hayo, Ruiru na Githurai yana garimoshi moja kuukuu la abiria linalohudumu hadi jijini Nairobi.

Pia, kuna magarimoshi kadhaa ya mizigo, ambapo eneo la Ruiru lina viwanda kadhaa.

Uzinduzi wa vituo hivyo, kwa baadhi ya wakazi unapokelewa kwa shime.

“Msongamano Thika Road umetuhangaisha kwa muda mrefu hususan tunaofanya kazi jijini Nairobi. Tunaomba mikakati murwa iwekwe ili kufanikisha usafiri na uchukuzi wake,” akapendekeza Reginnah Wairimu.

Mradi huo pia unaonekana kuimarisha maeneo hayo ambapo umevutia wawekezaji katika majumba ya makazi – kukodi na biashara. Ni kupitia maendeleo hayo, baadhi ya barabara zinazoelekea katika kituo cha Githurai zinawekwa lami, suala ambalo wahudumu wa tuktuk na bodaboda wanalipongeza.

“Ni ishara kwamba biashara ya usafiri na uchukuzi eneo hili itanoga,” akasema Mwara Muchangi mhudumu wa tuktuk. Mtaa wa Githurai una zaidi ya tukutuk 300 na maelfu ya bodaboda.