Vivian Nasaka Makokha ajiunga na Hakkarigucu Spor kwa mkataba wa mwaka mmoja

Vivian Nasaka Makokha ajiunga na Hakkarigucu Spor kwa mkataba wa mwaka mmoja

NA RUTH AREGE

BEKI wa pembeni wa Harambee Starlets Vivian Nasaka Makokha, amesaini mkataba wa mwaka mmoja na timu ya Hakkarigucu Spor ya Ligi Kuu ya Wanawake ya Uturuki.

Makokha anajiunga na timu hiyo kutoka kwa mabingwa wa sasa wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL) Vihiga Queens.

Aliiongoza Queens kunyakua taji la Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) jijini Nairobi mwaka 2021.

Mabingwa hao mara tatu wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL), waliwakilisha kanda ya Afrika Mashariki kwenye mchujo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa ya Wanawake yaani (CAF) nchini Misri mwezi wa Novemba 2021.

Makokha anasema yuko tayari kupambania klabu yake mpya msimu ujao.

“Timu yetu iko imara sana kwani ina wachezaji wazuri. Nimefurahi kufika hapa na ni mara yangu ya kwanza kufika Uturuki. Nina imani na timu yangu, kocha wangu na wachezaji wenzangu, natumai tutakuwa na msimu mzuri na tuchukue ubingwa,” alisema Makokha.

“Hakkari ni jiji dogo na zuri linalofanya watu kuwa wa wakarimu kwa kuwa wamenikaribisha vizuri,” aliongezea Makokha.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19, aliichezea Kenya katika ngazi ya juu wakati wa Mashindano ya CECAFA ya Wanawake ya 2019 na kombe la Uturuki la Wanawake 2020. Nchi zingine zilizoshiriki mashindano ya Uturuki ya wanawake ni pamoja na Hungary, Venezuela, Hong Kong, Romania, Uzbekistan, Ireland ya Kaskazini, Turkmenistan na Chile.

Pia alikuwemo kwenye kikosi cha Starlets kilichopangwa kumenyana na Crasted Cranes Uganda katika kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (AWCON) 2022.

Meneja wa Ufundi wa Hakkarigücü Cemile Timur anasema kuwa wameachana na takriban nusu ya wachezaji wa timu hiyo na kuimarisha kikosi na wachezaji wapya ambao anaamini watamsaidia kufikia lengo lake.

“Msimu uliopita, timu yetu ilikuwa nzuri, lakini tulikuwa na mapungufu. Tuliachana na karibu nusu ya timu na hivyo tumeimarisha kikosi chetu. Wachezaji wote tuliowaleta ni wazuri kwa kuwa ni wazoefu.”

“Tuliiongezea timu na kuchagua wachezaji wa kigeni kutoka Afrika, tena kutokana na uchambuzi wetu kuna wachezaji wa soka ambao tuliwafuata kupitia wasimamizi na kufanikiwa katika timu zao za taifa, tukaongeza wachezaji wanne wa kigeni kwenye kikosi chetu. Tuliendelea na wachezaji wetu wawili wa kigeni kutoka mwaka 2021,” aliongeza Timur.

Hakkaragucu Spor pia ni nyumbani kwa mshambuliaji wa Kimataifa wa Kenya, Mwanahalima Dogo Jereko.

Wakati huo huo mshambuliaji wa Starlets Marjoleen Nekesa amejiunga na klabu ya SK Slavia nchini Czech Republic kwa mkataba wa muda usiojulikana. Alichangia ushindi wa 8-0 dhidi Baník Ostrava kwa kufunga bao moja.

Naye mchezaji mwingine wa Starlets Fatuma Abubakar aliisaidia klabu yake ya Yei Joint Stars Fc ya Sudan Kusini kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya wanawake msimu wa 2021/22.

  • Tags

You can share this post!

Ruto awasilisha bungeni majina ya watu 22 aliopendekeza...

Waluke atorokea bungeni yeye na Wakhungu wakirudishwa jela...

T L