Habari Mseto

VIVIAN WANJIKU: Analenga kumpiku staa Priscilla Shirer kisanaa

February 8th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

ALIANZA kujituma katika masuala ya uigizaji tangu akiwa mdogo akishiriki filamu za Kikristo ikiwamo kuzaliwa kwa Yesu Kristo kati ya zingine. Hata hivyo, mwaka 2011 alionekana kuimarisha talanta yake alipoanza kuendeleza taaluma hiyo kama ajira.

Vivian Wanjiku Ritho anasema kimsingi hushiriki uigizaji akilenga kutumia nafasi hiyo kuhubiri neno ya Mungu kwa wafuasi wake.

”Haja yangu kushiriki muvi siyo mapato mbali huwa nasaka mwanya kutambuliwa na jamii baada ya kuona sura yangu kwenye runinga,” alisema na kuongeza kwamba ushiriki wake umefanikisha nia yake pakubwa.

Hata hivyo alisema mwanzo wake alipata nafasi kushiriki muvi tatu mfululizo bila mafanikio baada ya maprodyuza waliokuwa wakishughulikia kushindwa kuzikamilisha kwa kukosa mtaji.

Alianza kushiriki muvi akiwa maeneo ya nyumbani Nyahururu mwaka 2011 baada ya maprodyuza tofauti kumhusisha walipogundua talanta yake.

”Baada ya kutofaulu mara tatu nilivunjika moyo sana ingawa nilivutiwa na uigizaji tangu utotoni mwangu,” aliambia Taifa Leo Dijitali.

Mwaka 2013 aliingia jijini Nairobi akiamini angepata ajira ya uigizaji kwa urahisi, lakini alikutana na mafisi ambao hupenda kutumia jasho ya wasanii kujifaidi.

Mbali na uigizaji demu huyu (25) anafanya kazi katika makao makuu ya Kanisa la Kiangikana la All Saints Cathedral Karen,Nairobi.

Vivian ndiye mshirikishi mkuu kwa masuala ya vijana katika kanisa hilo. Mrembo huyu anasema muvi ya kwanza kupata mpenyo kupeperushwa kwa runinga ilifahamika kama ‘Unafiki’ iliyotengenezwa na Ngonyore Production.

”Bila kuongeza chumvi wala ladha yoyote hatua hiyo ilifanya kujihisi kwamba nina talanta ya uigizaji na kunitia motisha zaidi,” alisema.

Mwigizaji huyu kwa sasa anafanya kazi na brandi ya Israel Productions kati ya zingine ambapo muvi zao huonyeshwa kupitia Inooro TV.

Anasema analenga kunoa kipaji chake katika uigizaji mpaka ampiku mwigizaji wa kimataifa mzawa wa Marekani, Priscillar Shirer aliyetamba kupitia muvi ya ya Kikristo ya ‘War Room.

Staa huyo amefaulu kushiriki muvi chungu mzima zikiwamo ‘Bible Teacher,’ ‘I can only imagine,’ na ‘Overcomer,‘ kati ya zinginezo.

”Napenda sana kushiriki muvi na filamu zinazoangazia neno ya Mungu maana licha ya umri wangu kimsingi napenda kubadilisha maisha ya wanawake na vijana kwa jumla,” alisema na kuongeza muvi za Kikristo huwa nzuri kutazamwa na kila mtu.

Demu huyu mwenye tabasamu ya kuvutia ameshiriki muvi nyingi tu ikiwamo ‘Mbugi matu,’ iliyobahatika kurushwa kupitia Kameme TV.

Zingine ambazo hupeperushwa kupitia Inooro TV ni ‘Kirumi (Laana),’ Igai ria baba (mgao wa babangu),’ ‘Boss lady,’ ‘Jesu wa Ndumberi (Yesu wa Ndumberi),’ ‘Kiriro (kilio),’ na hivi karibuni ameshiriki ‘Kaba Gukua (Bora kufa),’ kati ya zingine. Anasema kando na kushiriki muvi pia filamu analenga kumiliki brandi yake miaka ijayo.

Anawataka waigizaji wanaoibukia kutolaza damu mbali wajitume na wawe wabunifu ili kufanikisha ndoto zao katika tasnia ya filamu na muvi.

Kadhalika, analia na serikali za Kaunti kote nchini hasa kuwazia kuwekeza katika sekta ya uigizaji ili kuwaokoa wenye vipaji mashinani.